Israel yafanya tena mashambulio ya anga magharibi mwa Syria
Katika kile kinachoonekana kuwa ni kuendeleza uchokozi wake, jeshi la utawala ghasibu wa Israel kwa mara nyingine limefanya mashambulizi ya anga katika maeneo ya mkoa wa Homs magharibi mwa Syria.
Duru za habari zimeripoti kwamba ndege za kivita za utawala huo katili zimefanya mashambulizi hayo asubuhi ya leo dhidi ya maeneo ya jeshi la Syria karibu na eneo la al-Qusair, magharibi mwa nchi hiyo. Hadi sasa hakijatangazwa kiwango cha hasara zilizosababishwa na shambulizi hilo.
Inafaa kuashiria kuwa, baada ya makundi ya kigaidi na ukufurishaji kushindwa vibaya katika maeneo tofauti na katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, jeshi la utawala haramu wa Israel liliongeza kiwango cha mashambulizi yake ya anga na mizinga dhidi ya maeneo ya jeshi la Syria kwa lengo la kulidhoofisha jeshi hilo la nchi hiyo na kuwapa nguvu magaidi.
Katika hatua ambayo ilikuwa haijawahi kushuhudiwa, jeshi la Syria hivi karibuni na katika kujibu hujuma za utawala wa Kizayuni, liliyashambulia vikali maeneo ya jeshi la Israel katika miinuko ya Golan na kuusababishia hasara kubwa utawala huo. Kiwango cha hasara kilichosababishwa na jibu la jeshi la Syria, kiliifanya Israel kuficha maeneo yaliyoshambuliwa katika miinuko hiyo, huku Tel Aviv ikitangaza kwamba haina nia ya kuingia vitani na taifa hilo wakati huu.