Israel yalegeza msimamo baada ya majibu makali ya wanamapambano wa Palestina
Baada ya wanamapambano wa Palestina kutoa majibu makali dhidi ya mashambulizi ya kivamizi ya hivi karibuni ya utawala wa Kizayuni, hatimaye baraza la masuala ya usalama la Israel limesema kuwa, utawala huo hauna nia yoyote ya kuukalia tena kwa mabavu Ukanda wa Ghaza.
Mtandao wa gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth limelinukuu baraza hilo likisema kuwa, utawala wa Kizayuni hauna nia kabisa ya kuuteka na kuukalia tena kwa mabavu Ukanda wa Ghaza bali hata linaunga mkono uamuzi wa Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa Israel na Evigdor Lieberman, waziri wa vita wa utawla huo dhalimu, wa kukomesha mashambulizi dhidi ya Ghaza.
Matamshi hayo yamekuja baada ya mawaziri wa mahakama na nishati wa utawala wa Kizayuni kutaka kufanyika mashambulizi makubwa ya pande zote kwa ajili ya kuukalia tena kwa mabavu Ukanda wa Ghaza na kuipindua serikali ya HAMAS katika ukanda huo.
Jumanne usiku wiki hii, makundi ya wanamapambano wa Palestina yalishambulia vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwa kutumia makombora 22, yakiwa ni mashambulizi kubwa zaidi kufanywa na wanamuqawama wa Palestina tangu baada ya vita vya siku 50 vya mwaka 2014.
Makubaliano ya kusimamisha vita yameanza kutekelezwa rasmi asubuhi ya leo Alkhamisi baina ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni kwa upatanishi wa Misri.