Maulamaa wa Palestina: Imam Khomeini MA alihuisha kadhia ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i45296-maulamaa_wa_palestina_imam_khomeini_ma_alihuisha_kadhia_ya_palestina
Msemaji wa Baraza la Maulamaa Wapalestina amesema: "Imam Khomeini MA, kwa kutangaza Ijumaa ya Mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds alihuisha kadhia ya Palestina."
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 01, 2018 23:40 UTC
  • Maulamaa wa Palestina: Imam Khomeini MA alihuisha kadhia ya Palestina

Msemaji wa Baraza la Maulamaa Wapalestina amesema: "Imam Khomeini MA, kwa kutangaza Ijumaa ya Mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds alihuisha kadhia ya Palestina."

Sheikh Mohammad Al Maud akizungumza Ijumaa katika mahojiano na Shirika la Habari la Rasaa alisema: "Kadhia ya Palestina ni kadhia ya Umma wa Kiislamu na Ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kutumia uwezo wake wote kusimama kidete na Palestina." Amongeza kuwa, "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi pekee ambayo imesimama kidete kutetea kadhia ya Palestina."

Mwanazuoni huyo wa Ahul Sunna amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetumia uwezo wake wote kuunga mkono harakati za mapambano ya Kiislamu za Palestina na Hizbullah ya Lebanon. Amebaini kuwa Iran inaunga mkono Palestina ambayo ni kadhia nambari moja katika ulimwengu wa Kiislamu.

Msemaji wa Baraza la Maulamaa wa Palestina ameashiria hatua ya Marekani kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv hadi Quds Tukufu na kuunga mkono mji huo kama mji mkuu wa utawala wa Kizyauni wa Israel na kusema hizo ni katika njama za Wazayuni dhidi ya Wapalestina. Hali kadhalika amesema hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel ni katika fremu ya njama hizo.

Kufuatia ubunifu wa Imam Khomeini MA, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ijumaa ya mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ilitangazwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds. Katika siku hii Waislamu na wapenda haki kote duniani hujumuika ili kubainisha kuchukizwa kwao na sera za kibaguzi za utawala wa Kizayuni wa Israel huku wakitangaza kuunga mkono malengo matukufu ya ukombozi wa Palestina.