Saudia yatishia kuishambulia kijeshi Qatar iwapo itanunua S-400 kutoka Russia
Mfalme Salman Bin Abdul Aziz Aal-Saud wa Saudi Arabia ametishia kuwa Riyadh itachukua hatua za kijeshi dhidi ya Qatar iwapo serikali ya Doha itaendelea na mpango wake wa kununua mfumo wa makombora wa S-400 kutoka Russia.
Kwa mujibu wa gazeti la Ufaransa la Le Monde, Mfalme Salman amemuandikia barua Rais Emmanuel Macron akimueleza kuhusu wasiwasi mkubwa alionao juu ya mazungumzo yanayoendelea kwa sasa kati ya Russia na Qatar, kuhusu mauzo ya mfumo huo wa kutungua makombora.
Mwezi uliopita wa Mei, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar alisema kuwa sababu iliyopelekea nchi yake kuwekewa mzingiro ni kutaka kuficha matatizo ya ndani ya Saudi Arabia, Imarati na Bahrain.
Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Aal-Thani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar amebainisha kuwa Doha siku zote inaunga mkono kufanyika mazungumzo lakini wakati huo huo hairuhusu kuvurugwa kivyovyote vile mamlaka ya kitaifa ya Qatar.
Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri zilikata uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar tangu mwezi Juni mwaka jana kwa kile kilichotajwa na nchi hizo kuwa ni kushindwa Doha kuwa pamoja na mrengo wa Kiarabu unaoongozwa na Riyadh na vile vile kufuatia nchi hizo kuituhumu Qatar kuwa inaunga mkono ugaidi.
Nchi hizo pia zimefunga mipaka yao ya majini, ardhini na angani na Qatar.