Iran: Hatutairuhusu Israel iufanye mwanasesere usalama wetu
Mshauri wa Masuala ya Kimataifa wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema katu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitouruhusu utawala wa Kizayuni wa Israel kuufanya mwanasesere usalama wake.
Hossein Amir-Abdollahian aliyasema hayo jana katika ujumbe aliouchapisha katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kufafanua kuwa: Utawala haramu wa Israel katu hauwezi kuruhusiwa kuvuruga usalama wa Iran na Mashariki ya Kati kwa ujumla."
Kadhalika amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuziunga mkono nchi rafiki na makundi ya muqawama katika eneo hili.
Mshauri wa Masuala ya Kimataifa wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu amebainisha kuwa, Baitul Muqaddas ni kibla cha kwanza cha Waislamu, na wala sio uwanja wa kufanya mauaji dhidi ya watoto wadogo wa Kipalestina.
Licha ya upinzani mkubwa wa kieneo na kimataifa, tarehe 14 Mei, serikali ya Marekani iliuhamishia katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu ubalozi wake uliokuweko Tel Aviv.
Sambamba na kuhamishiwa Baitul Muqaddas ubalozi huo, maandamano ya mamilioni ya Wapalestina yalifanyika katika mpaka wa Ukanda wa Gaza kwa anwani ya "Haki ya Kurejea" kwa lengo la kuvunja mzingiro lililowekewa eneo hilo na kuhakikisha malengo matukufu ya Wapalestina yanafikiwa, ambapo makumi ya Wapalestina waliuwa shahidi na jeshi katili la Israel.