Qatar yamteua balozi mpya maalumu kuhudumu Iran
(last modified Thu, 14 Jun 2018 07:48:26 GMT )
Jun 14, 2018 07:48 UTC
  • Qatar yamteua balozi mpya maalumu kuhudumu Iran

Sheikh Tamim bin Hamad, Amiri wa Qatar, amemteua Mohammed bin Hamad Al Hajri kuwa balozi mpya maalumu wa nchi hiyo katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Cheo cha balozi maalumu mwenye mamlaka kamili (extraordinary and plenipotentiary) ni cheo cha juu zaidi cha kidiplomasia ambacho balozi anaweza kupewa na hivyo kumfanya atambulike pia kama mjumbe maalumu.

Baada ya Oman, Qatar ndio nchi yenye uhusiano mzuri zaidi na Iran miongoni mwa nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi. Kinyume na Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar imekuwa ikijiepusha kuwa na msunguano katika uhusiano wake na Iran na badala yake imekuwa ikijitahidi kuwa na uhusiano mzuri na Jamhuri ya Kiislamu.

Katika kuwepo uhusiano huo mzuri, nchi mbili zimejitahidi kutoathiriwa na migogoro inayojiri katika  eneo lenye misuguano mikali la Mashariki ya Kati. Mbali na hayo kuna nukta kadhaa ambazo zimepelekea Qatar na Iran kutaka kuwa na uhusiano mzuri kama vile mpaka wa pamoja wa baharini na kuwa na eneo la pamoja na uchimbaji gesi baharini. Uhsiano wa nchi hizi mbili pia umeathiriwa na sera za Saudi Arabia katika eneo.

Kuna hali ya kutoaminiana katika uhusiano wa Iran na Saudia Arabia, ambayo pamoja na Uturuki zinahesabiwa kuwa washindani wakuu wa Iran katika eneo.

Sheikh Tamim bin Hamad, Amiri wa Qatar

Uhusiano wa Qatar na Saudi Arabia pia haujawahi kuwa kama uhusiano wa karibu wa Bahraini na Saudia au UAE na Saudia.

Qatar haiafiki hata kidogo tabia ya Saudi Arabia ya kujifanya ndiye kiranja wa eneo. Msimamo huo wa Qatar unashuhudiwa wazi katika mgogoro uliopo hivi sasa baina ya nchi za Kiarabu. Qatar inapinga vikali hatua ya Saudia kuingilia mambo ya ndani ya nchi zingine za Kiarabu na inasema hatua hizo zinahatarisha usalama wake. Hivi sasa tuko katika mwaka wa pili wa mgogoro wa nchi za Kiarabu ambapo Juni mwaka jana Saudia, Bahrain, na UAE pamoja na Misri zilitangaza kukata uhusiano na Qatar na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa nchi kavu, anga na baharini. Sababu kuu ya kuendelea mgogoro huo ni kuwa Qatar inasisitiza kulinda uhuru na mamlaka yake ya kujitawala na inakabiliana na sera za ubabe na kutaka kujitanua za Saudi Arabia.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Sultan bin Saad Al Muraikhi akizungumza katika kikao cha mawaziri wa nje wa nchi za Kiarabu mjini Cairo Disemba mwaka 2017 katika tamko la kinaya kwa Saudia Arabia alitamka wazi kuwa: "Iran ni nchi yenye heshima na hata siku moja haijatulazimisha kufungua au kufunga ubalozi wetu katika nchi hii au nchi ile."

Weledi wa mambo wanaamini kuwa Qatar imechukua msimamo wa kuwa na uhusiano mzuri na Iran katika eneo.

Kwa hakika, hatua ya Saudia kujiona kama kiranja wa eneo na uingiliaji wake wa masuala ya ndani ya nchi zingine kama vile Qatar  ni jambo ambalo limepelekea nchi nyingi zisiridhike na sera hizo. Katika upande mwingine, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza kufuata sera yenye msingi wa kutoingilia masuala ya ndani ya nchi zingine. Sera hii ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepelekea nchi kama vile Qatar kuwa na hamu ya kuimarisha uhusiano na Iran na hili ni suala ambalo limewakera na kuwakasirisha sana watawala wa Saudia. Katika kipindi cha mwaka mmoja ambapo Qatar imewekewa mzingiro na nchi nne zikiongozwa na Saudia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepinga na kulaani vikali hatua hiyo. Kutokana na kuwa na mpaka wa pamoja wa baharini na Qatar, Iran imekuwa na nafasi muhimu sana kuisaidia nchi hiyo kupungiza athari mbaya za mzingiro huo na vikwazo.

Hivi sasa kwa kumteua balozi maalumu nchini Iran, Amiri wa Qatar Sheikh Tamim ametambua nafasi muhimu na ya kipekee ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hivyo pasina kuzingatia mashinikizo ya kigeni anaimarisha uhusiano na Tehran huku akiipuuza kikamilifu Saudia. Hatua hii kwa mara nyingine inathibitisha wazi kuwa Saudia inazidi kushindwa na kupata pigo katika mgogoro ilioibua miongoni mwa nchi za Kiarabu dhidi ya Qatar.

Tags