Jun 15, 2018 06:50 UTC
  • Saudia yaendelea kutumia silaha zilizopigwa marufuku nchini Yemen

Ndege za kivita za Saudi Arabia zimelishambulia eneo la Khadhrawan katika mkoa wa Sa'ada kwa kutumia mabomu ya vishada yaliyopigwa marufuku kimataifa.

Mashambulizi hayo ya silaha zilizopigwa marufuku ya Saudi Arabia dhidi ya raia wa Yemen ni kielelezo cha kushindwa muungano wa kidhalimu unaoshirikiana na Saudia huko Yemen licha ya kusaidiwa na Marekani na chini ya kimya cha jamii ya kimataifa. Hii si mara ya kwanza kwa ndege za kivita za Saudia kushambulia maeneo ya raia wa Yemen kwa kutumia makombora na mabomu yaliyopigwa marufuku ya vishada. Mbinu ya kutumia silaha zilizopigwa marufuku dhidi ya raia wa Yemen inafanyika kwa shabaha ya kufanya uharibifu mkubwa zaidi na kuwatia woga raia na wanamapambano wa Yemen ili wasitishe mapambano ya kukabiliana na wavamizi wanaosaidiwa na Marekani, Uingereza na utawala haramu wa Israel. Aghlabu ya maeneo ya Yemen yameshambuliwa kwa mabomu na ndege za kivita za Saudi Arabia na washirika wake na mashambulizi hayo yanalenga madaraja, mahospitali, shule, barabara, misikiti na miundombinu ya nchi hiyo. 

Mahospitali na shule zinaharibiwa nchini Yemen

Utumiaji wa mabomu yaliyopigwa marufuku kama mabomu ya vishada, na yale ya foforasi na ya sumu unaofanywa na Saudi Arabia huko Yemen umesababisha maafa makubwa, na maeneo mengi ya Yemen sasa yamekuwa maabara ya kujaribia silaha zinazotengenezwa na nchi za Magharibi hususan Marekani na Uingereza. Mabumu ya vishada yaliyotengenezwa Marekani na Uingereza yanayotumiwa na Saudia dhidi ya raia wa Yemen yalipigwa marufuku kwa mujibu wa mkataba wa mwaka 2008 uliotiwa saini na nchi 108. Kwa kutilia maanani uhakika huo inaeleweka kwamba, Saudi Arabia inayotumia silaha hizo dhidi ya raia huko Yemen na Marekani na Uingereza zinazoiuzia Saudia silaha hizo ni watenda jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Dhamiri ya Kimataifa anasema Marekani na Uingereza zinaipatia Saudia silaha zilizopigwa marufuku na kwamba utumiaji wa silaha hizo huko Yemen ni kinyume cha sheria na jinai ya kivita. 

Watoto wa Yemen wanauawa bila ya hatia yoyote

Kwa sasa maeneo mengi ya Yemen yamejaa mabomu ya vishada ambayo hayajalipuka. Kutofanikiwa kwa mashambulizi ya pande zote ya watawala wa Riyadh huko Yemen na kuendelea kusimama kidete kwa raia wa nchi hiyo kumewafanya Aal Saudi watumie silaha zilizopigwa marufuku ili kuwatia woga Wayemeni. Haya yote yanafanyika kwa uungaji mkono wa nchi zinazodai ni watetezi wa haki za binadamu kama Marekani na Uingereza, suala ambalo linaweka wazi zaidi sura halisi ya haki za binadamu zinazotetewa na wakoloni hao.   

Tags