Jeshi la Israel lamuua shahidi mwandishi mwingine wa habari huko Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i130268-jeshi_la_israel_lamuua_shahidi_mwandishi_mwingine_wa_habari_huko_gaza
Mwandishi wa Televisheni ya Al-Quds Today ameuawa shahidi katika shambulizi la Israel huko Gaza na hivyo kuzidisha idadi ya waandishi wa habari waliouawa shahidi katika vita na mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na Israel katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2025-09-01T07:40:56+00:00 )
Sep 01, 2025 07:40 UTC
  •  Islam Abed
    Islam Abed

Mwandishi wa Televisheni ya Al-Quds Today ameuawa shahidi katika shambulizi la Israel huko Gaza na hivyo kuzidisha idadi ya waandishi wa habari waliouawa shahidi katika vita na mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na Israel katika Ukanda wa Gaza.

Mwandishi huyo kike, Islam Abed, aliuawa shahidi jana jioni wakati ndege ya kivita ya Israel ilipodondosha bomu katika mji wa Gaza. 

Ofisi ya vyombo vya habari huko Gaza imetoa taarifa na kulaani kushambuliwa kwa makusudi na kwa utaratibu maalumu waandishi wa habari wa Palestina na imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kukomesha mauaji na kuwalinda wale wanaofanya kazi katika vyombo vya habari.

Televisheni ya satelaiti ya al-Quds Today pia imelaani mauaji ya Bi Islam Abed katika mji wa Gaza.

Imeongeza kuwa, "mashine ya mauaji ya Israel haitafanikiwa kunyamazisha sauti zetu, sauti za wananchi wa Palestina".

Muungano wa Wanahabari wa Palestina (PJS) pia umelaani mauaji ya Abed. Muungano huo umezitaka taasisi za kimataifa za kutetea haki za binadamu na za vyombo vya habari kuchukua "hatua za haraka na zenye athari ili kuhakikisha kuwa viongozi wa Israel wanawajibishwa kwa jinai zao za mara kwa mara dhidi ya tasnia ya uandishi wa habari ya Palestina."

Waandishi wa habari watano wa Palestina, ikiwa ni pamoja na mpiga picha wa Reuters, Hossam al-Masri, waliuawa katika mashambulizi mawili ya moja kwa moja kwenye ya jeshii la Israel Nasser Medical Complex siku ya Jumatatu wiki iliiyopita.

Waandishi wa habari wasiopungua 200 wameuawa shahidi na jeshi la Israel tangu utawala huo ghasibu uanzishe vita na mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Gaza Oktoba 7, 2023.