Haaretz: Bahrain inataka kuanzisha uhusiano wa dhahiri na Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i46522-haaretz_bahrain_inataka_kuanzisha_uhusiano_wa_dhahiri_na_israel
Gazeti la Kizayuni la Haaretz limeashiria uhusiano wa siri kati ya utawala wa Aal Khalifa wa Bahrain na utawala ghasibu wa Israel na kufichua kwamba, viongozi wa Manama wanataka kuanzisha uhusiano wa dhahiri na Tel-Aviv.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 02, 2018 09:55 UTC
  • Haaretz: Bahrain inataka kuanzisha uhusiano wa dhahiri na Israel

Gazeti la Kizayuni la Haaretz limeashiria uhusiano wa siri kati ya utawala wa Aal Khalifa wa Bahrain na utawala ghasibu wa Israel na kufichua kwamba, viongozi wa Manama wanataka kuanzisha uhusiano wa dhahiri na Tel-Aviv.

Kwa mujibu wa gazeti hilo ni kuwa, hivi sasa viongozi wa Bahrain wanachunguza mazingira ya kuweka wazi uhusiano wao na utawala haramu wa Israel.

Gazeti hilo la Kizayuni linaeleza kwamba, licha ya kuwa Bahrain na Israel hazina uhusiano wa wazi, lakini pande hizo mbili zina manufaa ya pamoja ambayo yanawafanya viongozi wa Manama na Tel Aviv kuchukuua hatua za kukurubiana zaidi.

Mfalme wa Bahrain, Hamad bin Isa Al Khalifa

Gazeti hilo aidha limeashiria uungaji mkono wa Khalid bin Ahmad al-Khalifa, Waziri Mkuu wa Bahrain kwa uvamizi wa kijeshi wa Israel dhidi ya Syria miezi miwili iliyopita na kubainisha kwamba, hiyo ni ishara ya wazi ya kuanzishwa uhusiano wa wazi kati ya pande mbili.

Wakati huo huo, licha ya upinzani mkali wa wananchi na asasi mbalimbali za Baharain, mkutano wa 42 wa shughuli za Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO ulianza kufanyika nchini Bahrain tangu Juni 24 kwa kuhudhuria na ujumbe kutoka Israel.

Mkutano huo wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO unatarajiwa kuendelea kufanyika mjini Manama hadi Julai 4 mwezi huu.