UN, EU zaitaka Israel isibomoe kijiji cha Wapalestina Ukingo wa Magharibi
Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya zimeutaka utawala wa Kizayuni wa Israel usitishe mpango wake wa kubomoa kijiji cha Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Ofisi ya Nikolay Mladenov, Mjumbe wa Amani wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Mashariki ya Kati sambamba na kulaani kuendelea ubomozi wa nyumba za Wapalestina katika eneo la Abu Nuwar, imekosoa vikali mpango wa utawala huo ghasibu wa kukisawazisha na ardhi kijiji cha Khan Al-Ahmar, kilichoko mashariki mwa mji mtukufu wa Quds.
Wakati huo huo, taarifa ya Umoja wa Ulaya imesema kuwa, nchi za EU zinatumai kuwa Israel itaangalia upya azma yake hiyo ya kukisambaratisha kikamilifu kijiji hicho, chini ya Sheria ya Kimataifa ya Ubinadamu.
Kwa upande wake, Hanan Ashrawi, mwanachama wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO amesema mpango huo wa kukibomoa kikamilifu kijiji hicho ambacho wakazi wake wengi ni Wabedui, ni jinai ya kivita huku akiitaka jamii ya kimataifa kuingilia kati na kuzima mpango huo.
Naye Bruce Katz, rais wa Jumuiya ya Wapalestina na Mayahudi amesema mpango huo wa kutaka kukifuta kabisa kijiji cha Khan al-Ahmar ni sehemu ya mchakato mpana na kukiangamiza kizazi kizima cha Wapalestina na kughusubu ardhi zao.