Saudia yamwita nyumbani balozi wake wa Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i46671-saudia_yamwita_nyumbani_balozi_wake_wa_lebanon
Serikali ya Saudi Arabia imemwita nyumbani balozi wake Walid al-Bukhari, kutoka Beirut, mji mkuu wa Lebanon.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 09, 2018 21:53 UTC
  • Saudia yamwita nyumbani balozi wake wa Lebanon

Serikali ya Saudi Arabia imemwita nyumbani balozi wake Walid al-Bukhari, kutoka Beirut, mji mkuu wa Lebanon.

Kufuatia mwito huo, Al-Bukhari  amesimamisha vikao na shughuli zake zote mjini Beirut katika kujiandaa kurejea nyumbani. Gazeti la al-Akhbar la nchini Lebanon limeandika kuwa, baadhi ya ripoti zimedokeza kwamba Riyadh imekusudia kumtuma afisa wa kijeshi kuchukua nafasi ya Al-Bukhar nchini Lebanon. Itakumbukwa kuwa kwa muda mrefu ubalozi wa Saudia mjini Beirut ulisalia bila kuwa na balozi, ambapo baadaye ilimteua Walid al-Yaqub kuwa mwakilishi wake nchini humo.

Hatua ya kumwita yumbani balozi wake mjini Beirut inatokana na kufeli njama za Riyadh nchini Lebanon

Hata hivyo miezi minne baadaye Riyadh ilimpiga kalamu nyekundu Walid al-Yaqub na kumteua Walid al-Bukhari ambaye kwa miaka kadhaa alikuwa Beirut kama mwambata wa ubalozi huo kushika nafasi hiyo ambaye hata hivyo naye amevuliwa nafasi hiyo kwa sababu ambazo hazijatajwa. Baadhi ya weledi wa mambo wameyataja mabadiliko hayo ya kila mara kwa viongozi wa kidiplomasia wa Saudia kuwa yanayotokana na stratijia ya Lebanon. Kufeli njama ya kumtaka ajiuzulu kwa nguvu Saad Hariri, Waziri Mkuu wa Lebanon akiwa mjini Riyadh na kadhalika kushindwa makundi ya kisiasa yenye mfungamano na Saudia katika uchaguzi wa bunge uliopita nchini humo, ni miongoni mwa mambo yanayotajwa kuwa chanzo cha mabadiliko hayo ya Saudia nchini humo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.