UN yaitaka Israel isitishe uchokozi wake Ghaza
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameutaka utawala haramu wa Israel usitishe uchokozi wake katika Ukanda wa Ghaza.
Akizungumza Jumamosi, Guterres ambainisha wasiwasi wake kutokana na machafuko ya Ukanda wa Ghaza kuendelea kuwa hatari.
Aidha ametoa wito kwa pande zote kushirikiana na Umoja wa Mataifa ili kutafuta suluhisho la amani na kuzuia kuwa mbaya zaidi hali ya maafa ya kibinadamu katika Ukanda wa Ghaza.
Wito wa Guterres umekuja baada ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kuvurumisha makombora katika kituo cha Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, katika Ukanda wa Ghaza. Uchokozi huo ulikuja masaa kadhaa baada ya utawala huo wa Kizayuni kufikia mapatano ya usitishwaji vita kwa muda baina yake na makundi ya Palestina huko Ghaza.
Hamas pia ilithibitisha kuwepo mapatano hayo ambayo yalifikiwa baada ya kuibuka mapigano katika Ukanda wa Ghaza. Hamas imesema mapatano hayo yalifikiwa kufuatia jitihada za Umoja wa Mataifa.
Wakati huo huo jana kulifanyika mazishi ya Wapalestina wanne ambao waliuawa katika Ukanda wa Ghaza Ijumaa baada ya kufyatuliwa risasi na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Wapalestina hao waliuawa shahidi wakati walipokuwa wakishiriki maandmano ya amani ya 'Haki ya Kurejea'.
Tokea Machi 30 hadi sasa, Wapalestina karibu 150 wameuawa shahidi katika maandamano hayo ya amani baada ya kufyatuliwa risasi na wanajeshi wa utawala katili wa Israel huku wengine karibu 16,000 wakijeruhiwa.