Jeshi la Israel lashambulia Gaza, Wapalestina 3 wauawa shahidi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i47023-jeshi_la_israel_lashambulia_gaza_wapalestina_3_wauawa_shahidi
Kwa akali Wapalestina watatu wameuawa shahidi katika wimbi jipya la mashambulizi ya angani na nchi kavu ya jeshi katili la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya makazi ya raia katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 26, 2018 02:43 UTC
  • Jeshi la Israel lashambulia Gaza, Wapalestina 3 wauawa shahidi

Kwa akali Wapalestina watatu wameuawa shahidi katika wimbi jipya la mashambulizi ya angani na nchi kavu ya jeshi katili la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya makazi ya raia katika Ukanda wa Gaza.

Wizara ya Afya ya Gaza imeripoti kuwa, mbali na watu watatu kuuawa, wengine kadhaa wamejeruhiwa huku mmoja akiwa katika hali mahututi, baada ya wanajeshi wa Israel kuushambulia mji wa Beit Lahia na maeneo mengine ya Ukanda wa Gaza.

Utawala huo haramu umedai kuwa mashambulizi hayo ni ya kulipiza kisasi kutokana na risasi zilizofyatuliwa kutoka ukanda ulio chini ya mzingiro wa kibaguzi na kidhalimu. 

Hiivi karibuni duru za habari ziliarifu kwamba, kumefikiwa makubaliano ya kusitisha vita kati ya makundi ya Palestina na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel huko Ukanda wa Gaza kufuatia juhudi za Misri na duru za kimataifa.

Sehemu ya hujuma za Wazayuni dhidi ya Gaza

Hata hivyo, Fauz Barhum, Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema kuwa mashambulizi ya ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel katika maeneo ya wanamuqawama na yaliyowalenga raia wa Palestina katika maandamano ya Haki ya Kurejea ni ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha vita.

Tokea Machi 30 hadi sasa, Wapalestina karibu 150 wameuawa shahidi katika maandamano hayo ya amani baada ya kufyatuliwa risasi na wanajeshi wa utawala katili wa Israel huku wengine karibu 16,000 wakijeruhiwa.