Qatar yatoa wito wa kukomeshwa maafa na mgogoro wa Yemen
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar ametoa wito wa kuanzishwa mazungumzo ya kitaifa baina ya pembe tofauti nchini Yemen na kutoa kipaumbele kwa njia za kisiasa kwa ajili ya kukomesha mgogoro wa nchi hiyo.
Muhammad bin Abdurrahman Aal Thani ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: "Qatar inaendelea kushikilia msimamo wake thabiti wa kulitetea taifa la Yemen, kukombolewa taifa hilo na kukomeshwa maafa ya yake ambayo ndiyo makubwa zaidi katika historia ya sasa ya dunia."
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar ameongeza kuwa, hali ya sasa ya Yemen inalazimisha kupewa kipaumbele njia za kisiasa za utatuzi wa mgogoro wa nchi hiyo na kufanyika harakati za kimataifa za kulinda raia wa nchi hiyo, kwa sababu eneo la Mashariki ya Kati haliwezi tena kustahamili vita na mauaji zaidi.
Mwezi Machi mwaka 2015 Saudi Arabia ikiungwa mkono na Marekani, Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu, ilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya taifa la Yemen na hadi sasa makumi ya raia wa nchi hiyo wameuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Hata hivyo Saudia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao katika vita hivyo vinavyoendelea kwa miaka mitatu sasa kutokana na mapambano na kusimama kidete kwa taifa shupavu la Yemen.