WHO: Saudia imekiuka sheria za kimataifa kwa kuwaua raia wa Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i47659-who_saudia_imekiuka_sheria_za_kimataifa_kwa_kuwaua_raia_wa_yemen
Shirika la Afya Duniani WHO limesema mauaji ya raia wakiwemo watoto yaliyofanywa na ndege za kivita za Saudia katika eneo la Ad Durayhimi nchini Yemen ni sawa na shambulizi la mji wa Dahyan, huko Saada.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Aug 24, 2018 09:13 UTC
  • WHO: Saudia imekiuka sheria za kimataifa kwa kuwaua raia wa Yemen

Shirika la Afya Duniani WHO limesema mauaji ya raia wakiwemo watoto yaliyofanywa na ndege za kivita za Saudia katika eneo la Ad Durayhimi nchini Yemen ni sawa na shambulizi la mji wa Dahyan, huko Saada.

Jana Alhamisi ndege za kivita za Saudi Arabia zilidondoshea mabomu magari mawili ya wakimbizi Wayemen katika eneo la Ad Durayhimi katika mkoa wa Al Hudaydah magharibi mwa Yemen ambapo watu 31 wakiwemo watoto 22 na wanawake wameuawa.

Mwakilishi wa WHO nchini Yemen amebainisha masikitiko yake kufuatia shambulizi hilo ambalo limepelekea raia wasio na hatua kupoteza maisha na kusema: "Mauaji ya raia katika eneo la Ad Durayhimi ni sawa na shambulizi la mji wa Dahyan mkoani Saada na ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa."

Itakumbukwa kuwa tarehe tisa mwezi huu wa Agosti, ndege za utawala wa Saudia zilifanya shambulizi jingine la kinyama dhidi ya basi lililokuwa limewabeba wanafunzi wa Qur'an Tukufu katika msimu wa joto, shambulizi lililofanyika eneo la Dhahiyan la mkoa wa Saada, ambapo kutokana na hujuma hiyo watoto 55 waliuawa na wengine 77 walijeruhiwa. Jinai za utawala wa Saudia dhidi ya raia wa Yemen zinafanyika mbele ya kimya cha jamii ya kimataifa hususan Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Basi la shule ambalo lilikuwa limebeba watoto wakati lilipodondoshewa bomu na ndege za kivita za Saudia kaskazini mwa Yemen

Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kutoroka nchi. Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasiopungua 15,000 wasio na hatia.