Saudia inapanga njama ya kuvihamishia Lebanon vita ilivyoanzisha dhidi ya Yemen
Gazeti la Al-Akhbar limefichua kuwa Saudi Arabia inapanga njama mpya ya kuvihamishia Lebanon vita ilivyoanzisha dhidi ya Yemen.
Gazeti hilo linalochapishwa nchini Lebanon limeandika katika toleo lake la leo kuwa kwa mujibu wa ripoti za siri, wasaidizi wa Muhammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia wametoa ushauri katika kikao cha siri walichofanya na kiongozi huyo wa vita vya Yemen kuhamishiwa nchini Lebanon.
Al-Akhbar limeongeza kuwa kikao hicho kilichohudhuriwa na maafisa kadhaa wa utawala wa Aal Saud akiwemo waziri wa mambo ya nje Adel al-Jubeir na mkuu wa shirika la intelijensia la Saudia Khalid al-Hamidan, kilijadili matokeo ya kisiasa na kijeshi ya kukombolewa maeneo ya kusini mwa Syria na jeshi la nchi hiyo na vilevile matokeo ya mapigano ya hivi karibuni nchini Yemen na taathira zake hasi kwa nafasi ya Saudia katika nchi za Kiarabu na Kiislamu na jinsi ya kufidia athari hizo.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, baada ya kikao hicho, wimbi la hujuma za vyombo vya habari vya Saudi Arabia dhidi ya Lebanon lilianza, kubwa zaidi zikiwa ni hujuma za gazeti la Akkadh lililochapisha makala yenye anuani isemayo: "Lebanon; subira yetu ina mpaka."
Katika makala yake hiyo, Khalid Sulaiman, mwandishi wa magazeti aliye karibu na ofisi ya mrithi wa ufalme wa Saudia ameandika kuwa: hatua kinzani za Lebanon haziwezi kuachwa ziendelee; serikali ya nchi hiyo inachukua misimamo isiyo na athari yoyote; wakati umewadia wa kujulikana msimamo wa ndani na wa nje wa Lebanon.../