Qatar yakerwa na jinai za kivita zinazotendwa na Saudia nchini Yemen
(last modified Wed, 29 Aug 2018 14:55:01 GMT )
Aug 29, 2018 14:55 UTC
  • Qatar yakerwa na jinai za kivita zinazotendwa na Saudia nchini Yemen

Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar amekosoa ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na jinai za kivita zinazotendwa na Saudia na Imarati nchini Yemen.

Mohammed bin Abdulrahman Al Thani ameyasema hayo kupitia ujumbe alioutuma katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na Yemen ni yenye kutia wasi wasi mkubwa na inapingana na sheria za kimataifa zinazopiga vita jinai za kivita, ukiukaji wa haki za binaadamu na kiakhlaqi. Aidha Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar ametaka kufanyika mazungumzo ya kitaifa kati ya makundi mengine nchini Yemen kwa lengo la kuzuia umwagikaji damu zaidi sambamba na kurejeshwa usalama nchini humo.

Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar

Hii ni katika hali ambayo wataalamu watatu wa Umoja wa Mataifa na katika ripoti yao ya kwanza kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameashiria hasara na uharibifu vinavyotokana na mashambulizi ya anga ya muungano vamizi wa Saudia dhidi ya Yemen katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Aidha wataalamu hao sambamba na kuelezea kwamba kuna uwezekano wa serikali za Saudi Arabia na Imarati kutambuliwa kuwa wahusika wa jinai za kivita nchini Yemen, waliitaka jamii ya kimataifa kuzuia kuiuzia Saudia silaha na zana za kijeshi. Inafaa kuashiria kuwa, jinai za Saudia kwa kushirikiana na waitifaki wake wa Marekani, Israel, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi huko Yemen zinafanyika mbele ya kimya cha jamii ya kimataifa.

Tags