Operesheni za kuikomboa Halab Syria zinaendelea
Waziri wa Habari wa Syria amesema kuwa, opereseheni za jeshi la nchi hiyo na vikosi vya wananchi dhidi ya magenge ya kigaidi, zingali zinaendelea.
Televisheni ya al Mayadeen imemnukuu Omran al-Zoubi akisema hayo leo na kuongeza kuwa, operesheni za ukombozi wa mji wa Halab zinaendelea kuwafurushwa magaidi nje ya mji huo.
Waziri wa Habari wa Syria ameongeza kuwa, baadhi ya miji mikuu ambayo ni vibaraka wa Washington hususan Ankara (mji mkuu wa Uturuki) na Aman (mji mkuu wa Jordan) haina njia nyingine ila kukubali ukweli wa mambo unaojiri huko Syria na iache kuwaunga mkono magaidi.
Amesema, ujumbe wa wapinzani unaofanya mazungumzo na serikali ya Syria haupaswi kuyajumuisha magenge ya kigaidi.
Omran al-Zoubi ameongeza kuwa, hakuna vikosi vya nchi za kigeni vinavyopigana bega kwa bega na vikosi vya Syria katika medani za mapambano, na wakati wowote vikosi vya nchi za kigeni kama vile Iran vitakapoanza kushiriki kwenye medani za mapambano huko Syria, Damascus haitaona tabu hata kidogo kuutangazia ulimwengu suala hilo.