Maandamano ya Wapalestina mbele ya ubalozi mdogo wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i47923-maandamano_ya_wapalestina_mbele_ya_ubalozi_mdogo_wa_marekani
Idadi kubwa ya Wapalestina wamefanya maandamano mbele ya ubalozi mdogo wa Marekani katika mji wa Ramallah katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan wakilalamikia hatua ya serikali ya Washington ya kukata misaada yake kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Ajili ya Wapalestina (UNRWA).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 05, 2018 22:25 UTC
  • Maandamano ya Wapalestina mbele ya ubalozi mdogo wa Marekani

Idadi kubwa ya Wapalestina wamefanya maandamano mbele ya ubalozi mdogo wa Marekani katika mji wa Ramallah katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan wakilalamikia hatua ya serikali ya Washington ya kukata misaada yake kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Ajili ya Wapalestina (UNRWA).

Isam Bakr ambaye ni mjumbe wa Idara ya Masuala ya Siasa ya Chama cha Wananchi wa Palestina amesema wakati wa maandamano hayo kwamba, Wapalestina wanafanya maandamano mbele ya ubalozi wa Marekani kupinga uamuzi wa Washington dhidi ya UNRWA na wataendelea kusimama kidete kupinga juhudi za kutaka kutekeleza mpango uliopewa jina la Muamala wa Karne. 

Wiki kadhaa zilizopita Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani ilitangaza kuwa nchi hiyo imekata misaada yake yote kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Ajili ya Wapalestina (UNRWA). Tarehe 6 Disemba mwaka 2017 Rais Donald Trump wa Marekani alianza kutekeleza mpango wa "Muamala wa karne" kwa kuutangaza mji mtakatifu unaokaliwa kwa mabavu wa Quds kuwa ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel. Siku hiyo hiyo Trump alitangaza uamuzi wake wa kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv na kuupeleka Quds, uamuzi ambao ulitekelezwa kivitendo tarehe 14 Mei mwaka huu. Marekani inatumia njia zote hata za kinyama na kikatili kwa ajili ya kutekeleza mpango huo mchafu ikiwa ni pamoja na njia ya kuzidisha mashinikizo na kuwatesa kwa njaa wakimbizi wa Palestina. 

Maandamano ya Wapalestina dhidi ya Marekani.

Kadiri muda unavyopita ndivyo sura ya mpango wa Muamala wa Karne inavyodhihirika wazi zaidi na pendekezo la Donald Trump la kuundwa Muungano wa Palestina na Jordan unafichua zaidi njama za Marekani dhidi ya taifa la Palestina. Katika mpango huo suala la wakimbizi limetatuliwa kwa kupatiwa ardhi mbadala nje ya Palestina huku haki ya wakimbizi Wapalestina ya kurejea nchini mwao ikifutwa kabisa. Jordan na baadhi ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu zimepangwa kuwa ziwe ndiyo nchi na ardhi ya Wapalestina. 

Gazeti la Haaretz la Israel siku chache zilizopita lilitoa ripoti likifichua vipengee vya mpango wa Muamala wa Karne na kuandika kuwa, mpango huo kimsingi ulipendekezwa na Israel. Ripoti hiyo inasema kuwa, kwa mujibu wa pendekezo hilo eneo la Ukingo wa Magharibi  bila ya kujumuisha Quds (Jerusalem) litawekwa chini ya usimamizi wa Jordan, na Israel itajitangazia kutwaa Quds na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zote za Palestina.

Mpango huo umenyamazia kimya hatima ya eneo la Jordan Valley au Bonde la Jordan na kwamba, je eneo hilo litakuwa chini ya mamlaka ya utawala wa ghasibu wa Israel au Muungano wa Palestina na Jordan? Mpango huo wa Wazayuni utaiunganisha ardhi ya Palestina na Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel), na wakazi wa Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi watapelekwa Jordan na eneo la Sinai huko Misri. Kwa maana kwamba, Palestina nzina isipokuwa sehemu ndogo ya Ukanda wa Gaza, itachukuliwa na Wazayuni maghasibu.

Wapalestina wanapinga njama za Marekani.

La kusikitisha zaidi ni kuwa nchi za Magharibi, badala ya kulisaidia taifa la Palestina na kulaani uhalifu huo wa Marekani, zimekuwa mshirika wa Washington katika mpango huo mchafu na hatari na zinafanya jitihada za kuwalazimisha Wapalesrina wakubaliane nao. Suala hili linaonesha kuwa, harakati za Marekani dhidi ya taifa la Palestina zimeingia katika awamu hatari sana na wakati huo huo linaweka wazi jinsi Wamarekani walivyo tayari kuhudumia malengo haramu ya Wazayuni hata kama ni kwa gharama ya kuliangamiza taifa zima la Palestina. Hapana shaka kuwa hali kama hii inachochea zaidi hisia za kuipinga Marekani kati ya Wapalestina, na maandamano yaliyofanyika mbele ya ofisi ya ubalozi mdogo wa Marekani mjini Ramallah ni kielelezo cha hisia za aina hiyo.