Haniya: HAMAS katu haitautambua utawala wa Kizayuni
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema Ukanda wa Gaza umeingia kwenye vita kamili vya kiusalama na kijeshi na shirika la intelijensia na usalama wa ndani la utawala wa Kizayuni Shabak.
Ismail Haniya amesisitiza kuwa harakati ya Hamas katu haitautambua utawala wa Kizayuni wa Israel na wala haitafikia nao mwafaka.
Haniya amebainisha kuwa, Wapalestina hawatafumbia macho hata shubiri moja ya ardhi yao kwa sababu Quds ni milki ya Wapalestina na kwa sababu hiyo Wapalestina kamwe hawataruhusu kutekelezwa mpango wa mapatano wa Marekani ujulikanao kama Muamala wa Karne.
Kwa mujibu wa mpango huo wa kihaini wa Marekani, mji wa Baitul Muqaddas utakabidhiwa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, wakimbizi Wapalestina hawatakuwa na haki tena ya kurejea kwenye ardhi zao za jadi na nchi ya Palestina itakuwa sehemu zilizobaki tu za ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza.
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas amesema: Muqawama ndiyo njia ya mkato zaidi ya kuyakomboa matukufu ya Kiislamu Palestina kutoka kwenye makucha ya Wazayuni maghasibu.
Ismail Haniya amesisitiza kwamba Hamas itaendelea kushikamana na njia ya mapambano na muqawama wa kukabiliana na adui wa Kizayuni na kueleza pia kinagaubaga kuwa, harakati hiyo inapinga kuanzisha uhusiano wowote wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.../