Saudia yanunua mfumo wa makombora kutoka Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i48112-saudia_yanunua_mfumo_wa_makombora_kutoka_israel
Saudi Arabia imeripotiwa kununua mfumo wa ngao ya makombora kutoka utawala wa Kizayuni wa Israel, katika hali ambayo ripoti zinasema tawala mbili hizo zipo mbioni kuweka wazi na kuimarisha uhusiano wao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 13, 2018 09:22 UTC
  • Saudia yanunua mfumo wa makombora kutoka Israel

Saudi Arabia imeripotiwa kununua mfumo wa ngao ya makombora kutoka utawala wa Kizayuni wa Israel, katika hali ambayo ripoti zinasema tawala mbili hizo zipo mbioni kuweka wazi na kuimarisha uhusiano wao.

Duru za ngazi za juu za kidiplomasia zimeiambia tovuti ya habari ya Imarati ya Khaleejonline kwamba, utawala wa Aal-Saud umefanikiwa kununua mfumo huo wa ngao ya makombora kutoka Tel Aviv kutokana na upatanishi wa Marekani.

Awali utawala wa Kizayuni wa Israel ulikuwa umekataa kuuuzia utawala wa Riyadh mfumo huo wa makombora ukidai kuwa hauwezi kufunga mkataba wowote wa mauzo ya silaha na nchi za Kiarabu eti kwa kuwa huko ni kuhatarisha maslahi yake katika eneo.

Inaarifiwa kuwa, makubaliano hayo ya mauzo ya mfumo huo wa  makombora wenye kugharimu makumi ya mamilioni ya dola yataanza kutekelezwa mwezi Disemba, baada ya Saudia kukamilisha malipo

Muhammad bin Salman Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia (kushoto) mwezi Septemba mwaka jana alifanya safari ya siri huko Israel ambapo alikutana na viongozi wa ngazi za juu wa utawala huo, ikiwa ni katika jitihada za kuboresha uhusiano wa Riyadh na Tel Aviv.

Vyanzo vya habari vimedokeza kwamba, Saudia imenunua mfumo huo kwa shabaha ya kujikinga na makombora ya balestiki yanayovurumishwa kila uchao na wanaharakati wa Ansarullah wa Yemen.

Mwaka uliopita, gazeti moja la Kizayuni lilifichua kuwa, katika mkataba wa mabilioni ya dola wa ununuzi silaha baina ya Marekani na Saudia, baadhi ya mashirika ya uundaji silaha ya Israel yalianishwa kuwa yangestafidi na makubaliano hayo.