'Saudia inawashikilia wanaharakati 2,500 wa upinzani'
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i48186-'saudia_inawashikilia_wanaharakati_2_500_wa_upinzani'
Shirika la kutetea haki za wafungwa la Prisoners of Conscience limesema kuwa, watawala wa Saudi Arabia wanawazuilia wanaharakati zaidi ya 2,500 wa upinzani, wakiwemo wanazuoni wa Kiislamu na waandishi wa habari.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 17, 2018 02:21 UTC
  • 'Saudia inawashikilia wanaharakati 2,500 wa upinzani'

Shirika la kutetea haki za wafungwa la Prisoners of Conscience limesema kuwa, watawala wa Saudi Arabia wanawazuilia wanaharakati zaidi ya 2,500 wa upinzani, wakiwemo wanazuoni wa Kiislamu na waandishi wa habari.

Katika taarifa iliyotumwa na shirika hilo kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter: Wanaharakati 2,613 wakiwemo wanazuoni wa Kiislamu, majaji, waandishi wa habari, na wakili wanaoonekana kuwa wapinzani wa utawala huo wa Kiukoo wanaendelea kuzuiliwa katika mazingira magumu katika jela za Aal-Saud.

Asasi hiyo isiyokuwa ya kiserikali ya kutetea haki za binadamu nchini Saudia imebainisha kuwa, Khalid al-Alamaki, mwandishi wa habari mashuhuri nchini humo anazuiliwa na vyombo vya usalama nchini humo tangu Septemba 27 mwaka jana, pasina kuambiwa mashitaka yanayomkabili.

Ukandamizaji wa Aal-Saud dhidi ya wanaharakati wa upinzani

Shirika hilo limesema kukamatwa na kuzuiliwa wanaharakati wa kisiasa nchini humo ni sehemu ya mbinyo na ukandamizaji unaofanywa na watawala wa Riyadh wakiongozwa na Mrithi wa Kiti cha Ufalme, Mohammed bin Salman kwa muda sasa.

Baada ya kupata nguvu harakati za kudai mageuzi zilizotokea katika nchi za Kiarabu hapo mwaka 2011, Saudi Arabia ilikumbwa la maandamano na upinzani dhidi ya serikali katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Maandamano hayo yalishadidi zaidi katika maeneo ya mashariki mwa Saudia ambayo yana idadi kubwa ya Waislamu wa madhehebu ya Shia.