Katibu Mkuu wa Ansarullah: Wayemeni katu hawatasalimu amri kwa adui
Katibu Mkuu wa Ansarullah ya Yemen, Abdulmalik Badruddin amesema: Licha ya mauaji na jinai zote anazozifanya adui, hatoweza katu kuifanya Yemen isalimu amri.
Abdulmalik Badruddin aliyasema hayo jana mbele ya umati mkubwa wa waandaamanaji katika mji mkuu wa Yemen Sana'a ambapo alisisitizia tena uungaji mkono wake kwa muqawama na wananchi huru wa Yemen wanaopambana na ubeberu wa Marekani.
Katibu Mkuu wa harakati ya Ansarullah aidha ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye medani za vita za magharibi ya nchi kukabiliana na maadui.
Abdulmalik Badruddin amesisitiza kuwa kukabiliana na ubeberu wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati na kupambana na utawala ghasibu wa Kizayuni unaoikalia Quds tukufu kwa mabavu ni jambo muhimu sana.
Wakati huohuo Mufti wa Yemen Allamah Shamsuddin Sharafuddin amesema, ni wajibu kisharia kupambana na maadui na wavamizi na ametoa bishara ya ushindi kwa wananchi wa Yemen katika vita visivyo na mlingano vya kukabiliana na muungano wa Kiarabu na Kimarekani.
Saudi Arabia, ikisaidiwa na Marekani, utawala haramu wa Israel, Imarati na nchi nyingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen mwezi Machi mwaka 2015; na hadi sasa maelfu ya raia wasio na hatia wa nchi hiyo wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.../