Mamilioni ya wafuasi wa Ahlul-Bayt (as) washiriki maombolezo ya Ashura
(last modified Tue, 16 Jul 2024 11:37:48 GMT )
Jul 16, 2024 11:37 UTC
  • Mamilioni ya wafuasi wa Ahlul-Bayt (as) washiriki maombolezo ya Ashura

Mamilioni ya Waislamu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na maeneo mengine ya dunia leo wameshiriki katika maombolezo ya kumbukumbu ya Ashura ya kukumbuka siku ya kuuliwa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (a.s).

Ashura ni mwezi 10 Mfunguo Nne, Muharram, ambayo mwaka huu imesadifiana na leo Jumanne tarehe 16 Julai, 2024.

Imam Husain AS aliuawa shahidi kikatili na kinyama mwaka wa 61 Hijria katika jangwa la Karbala nchini Iraq baada ya kuongoza mapambano ya kishujaa ya ushindi wa damu mbele ya upanga.

Waombolezaji hapa nchini Iran wakiwa wamevaa nguo nyeusi, kama ishara ya huzuni na majonzi, walikuwa wakibubujikwa na machozi kwa kukumbuka dhulma iliyofanywa na madhalimu dhidi ya kizazi bora cha Mtume Muhammad (saw).

Wairani wanaoshiriki katika maombolezo ya Siku ya Ashura husikiliza hotuba na mashairi kuhusiana na masaibu yaliyomkumba Imam Hussein AS huko Karbala.

 

Mapambano ya Karbala ya Imam Hussein (a.s) na wafuasi wake watiifu yalitokea mwaka 61 Hijria, na watukufu hao walipigana kishujaa katika vita vya kidhulma dhidi ya maelfu ya wanajeshi wa khalifa wa Bani Umayyah, Yazid mwana wa Muawiya, mwana wa Abu Sufyan ambaye alikuwa adui mkubwa wa Mtume Muhammad (saw) na Waislamu na ambaye alitambulika kwa ulevi na kucheza kamari.

Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote na kwa kila mpenda haki na ukombozi duniani kwa mnasaba wa kukumbuka msiba huu mkubwa uliomfika Bwana Mtume Muhammad SAW na Uislamu kiujumla.