Jul 16, 2024 02:51 UTC
  • Jumanne, tarehe 16 Julai, 2024

Jumanne tarehe 10 Muharram 1446 Hijria, sawa na Julai 16 mwaka 2024.

Katika siku kama hii ya leo miaka 1388 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Uislamu na mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na majeshi ya batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq. Siku hii inajulikana kwa jina la A'shuraa. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili ili kuilinda dini ya Allah SW.

Hamasa ya Karbala ilikuwa dhihirisho la mambo mawili makuu. Kwanza ni ujasiri, ushujaa, moyo wa kujitolea, uaminifu pamoja na kuyapokea kwa moyo mkunjufu mauti ya kuuawa shahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, sifa walizojipamba nazo wapiganaji wachache wa jeshi la haki wakiongozwa na Imam Hussein AS dhidi ya Yazid bin Muawiya. Pili ni upeo wa ukatili, udhalimu na unyama ulioonyeshwa na jeshi batili la Yazid bin Muawiya.

Baada ya kupambana kishujaa, hatimaye mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi katika siku kama ya leo akiwa pamoja na watu wengine wa familia ya Mtume (saw), na wafuasi wake waaminifu. 

Siku kama ya leo miaka 134 iliyopita James Parkinson aligundua ugonjwa wa Parkinson na namna unavyotokea.

Kwa sababu hiyo ugonjwa huo ulipewa jina la tabibu huyo. Dalili za ugonjwa huo ni kama vile kutetemeka sana na kwa muda mrefu kwa ulimi, kichwa na mikono na kushindwa kuvuta miguu wakati wa kutembea hususan katika kipindi cha uzeeni na pia kukakamaa misuli katika sehemu yoyote ya mwili.

Ugonjwa wa Parkinson unasababishwa na baadhi ya matatizo katika ubongo na hadi kufikia sasa hakuna dawa mujarabu iliyopatikana kwa ajili ya kutibu maradhi hayo. 

James Parkinson

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita Baraza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilianza rasmi kazi zake.

Baraza hilo liliundwa kwa mujibu wa kipengee namba moja cha Katiba ya Iran kwa shabaha ya kulinda Sharia za Kiislamu na Katiba na kuhakikisha kwamba sheria zote zinazopasishwa hapa nchini hazipingani na viwili hivyo. Baraza hilo linaundwa na wataalamu 6 wa elimu ya fiqhi wanaoteuliwa na Kiongozi Mkuu wa Iran na wataalamu 6 wa sheria wanaoteuliwa na Idara ya Mahakama na kupasishwa na Bunge.

Kazi kuu ya baraza hilo ni kuhakikisha kwamba, sheria zote zinazopasishwa na Bunge haziendi kinyume na Sheria za Uislamu.

Siku kama ya leo miaka 16 iliyopita Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon kwa mara nyingine tena ilifanikiwa kupokea mateka watano na miili ya karibu mashahidi 200 wa Kilebanoni kutoka kwa utawala wa Kizayuni.

Ubadilishanaji huo wa miili na mateka hao ulifanyika kufuatia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya pande mbili hizo kwa usimamizi wa serikali ya Ujerumani.

Nukta ya kushangaza katika oparesheni hiyo ni hii kwamba vyombo vya usalama na ujasusi vya utawala wa Kizayuni hadi dakika ya mwisho havikuwa na habari kwamba wanajeshi wake wawili waliuawa mwanzoni mwa mapigano kati ya jeshi la utawala wa Kizayuni na wapiganaji wa Huzbullah.

Shakhsia wengine kutoka makundi ya mapambano ya Lebanon pia walikuwa miongoni mwa mateka walioachiwa huru na utawala wa Kizayuni. Shakhsia muhimu zaidi kuliko wote alikuwa Samir Qantar ambaye alipoteza karibu miaka 30 ya umri wake akiwa katika jela za utawala wa Kizayuni. 

Samir Qantar

Na katika siku kama hii ya leo miaka 9 iliyopita alifariki dunia qarii mashuhuri wa Misri, Sheikh Sayyid Mutawalli Abdul Aal.

Alizaliwa Aprili 1947 katika familia ya wachamungu nchini Misri na aliweza kuhifadhi Qur'ani Tukufu kikamilifu akiwa na umri wa miaka 12.

Alianza kujifunza qiraa ya Qur'ani Tukufu kwa kuiga mitindo ya maustadhi bingwa kama vile Sheikh Abdulbasit Abdusamad na Sheilh Mustafa Ismail.

Katika umri wake uliojaa baraka za Qur'ani, Sayyid Mutawalli Abdul Aal alitembelea nchi nyingi duniani kama qarii na pia jaji wa mashindano ya Qur'ani. Alifariki dunia Julai 16, 2015 akiwa na umri wa miaka 68.

Sayyid Mutawalli Abdul Aal

 

Tags