Jordan yataka Israel ijiunge na mkataba wa NPT
Dakta Khalid Toukan Mkuu wa Kamisheni ya Nishati ya Nyuklia ya Jordan ametaka utawala wa Kizayuni wa Israel ujiunge na mkataba unaopiga marufuku uenezaji na usambazaji wa silaha za nyuklia (NPT).
Dakta Toukan amesema katika Mkutano Mkuu wa 62 wa Wakala wa KImataifa wa Nishati ya Nyuklia mjini Vienna kuwa taasisi zote za nyuklia za utawala huo zinapasa kuwa chini ya usimamizi wa wakala wa IAEA kwa lengo la kuwa na eneo lisilo na silaha za nyuklia na kurejesha amani na usalama duniani.
Dakta Toukan ameashiria kuwa miongozo ya wakala wa IAEA ni miongoni mwa masuala ya msingi katika jitihada za kimataifa za kuzuia kuenea silaha za nyuklia na kuongeza kuwa silaha za aina hiyo na nyinginezo za maangamizi ya umati ni hatari kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa na wa eneo la Mashariki ya Kati. Mkuu wa Kamisheni ya Nishati ya Atomiki ya Jordan ameitolea wito jamii ya kimataifa kufanya juhudi za kulifanya eneo la Mashariki ya Kati kuwa eneo pasina na silaha za nyuklia na za maangamizi ya umati.
Itafahamika kuwa Israel ni utawala pekee unaomiliki mabomu ya nyuklia katika Mashariki ya Kati. Licha ya utawala huo kutojiunga na mkataba wa NPT na kutoonyesha ushirikiano wowote kimataifa kuhusu silaha hizo za nyulia, lakini unaungwa mkono na madola makubwa duniani.
Ni dhahir shahir kuwa silaha za nyuklia zinazomilikiwa na Israel ni ushahidi wa miamala na vigezo vya undumakuwili vya madola makubwa ya Magharibi na hatua yao ya kutotii sheria zinazopiga marufuku uenezaji na usambazaji wa silaha za nyuklia ulimwenguni.