Syria yasisitiza kuwa itaendelea kuimarisha uhusiano wake wa kiuchumi na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i48925-syria_yasisitiza_kuwa_itaendelea_kuimarisha_uhusiano_wake_wa_kiuchumi_na_iran
Katibu Mkuu wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Syria amesema kuwa, kuna haja ya kuondolewa vizuizi vyote hata vidogo vidogo katika juhudi za kuimarisha uhusiano wa pande zote wa kiuchumi baina ya nchi mbili ndugu za Iran na Syria.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Oct 20, 2018 12:20 UTC
  • Syria yasisitiza kuwa itaendelea kuimarisha uhusiano wake wa kiuchumi na Iran

Katibu Mkuu wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Syria amesema kuwa, kuna haja ya kuondolewa vizuizi vyote hata vidogo vidogo katika juhudi za kuimarisha uhusiano wa pande zote wa kiuchumi baina ya nchi mbili ndugu za Iran na Syria.

Mohammad Hamshou amesema hayo leo katika kongamano la ustawi wa ushirikiano wa kiuchumi baina ya Iran na Syria uliofanyika hapa Tehran na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapewa kipaumbele katika ujenzi mpya wa Syria.

Katibu Mkuu huyo wa umoja wa wafanyabiashara wa Syria amegusia pia ushirikiano mzuri uliopo baina ya Tehran na Damascus katika sekta ya uzalishaji magari na kuongeza kuwa, nchi hizo mbili zinaweza kushirikiana zaidi pia katika masuala kama ya usafiri na uchukuzi, mifumo ya benki, utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uzalishaji wa bidhaa n.k.

Mji wa Raqqa wa Syria ulivyoharibiwa vibaya na mashambulizi ya Marekani na magaidi. Syria sasa imefungua milango ya kuijenga upya nchi hiyo baada ya kuzidiwa nguvu magaidi

 

Vile vile amesisitiza kuwa, kuna haja ya kufanyika maonyesho mengi ya pamoja ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya nchi hizi mbili.

Kongamano la siku mbili la ushirikiano wa kibiashara baina ya Iran na Syria limeanza leo hapa Tehran kwa kushirikisha wanaharakati na vigogo wakubwa wa kiuchumi wa pande hizi mbili.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inahesabiwa kuwa moja ya waungaji mkono wakubwa wa taifa la Syria katika mgogoro liliobebeshwa taifa hilo la Kiarabu tangu mwaka 2011.