Hizbullah ya Lebanon yataka kuundwa serikali mpya haraka iwezekanavyo
Viongozi wa ngazi ya juu wa harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Lebanon Hizbullah wametaka kuundwa haraka iwezekanavyo serikali mpya nchini humo na kupatiwa ufumbuzi hitilafu zilizosalia.
Sheikh Naim Qassim Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa kuundwa serikali mpya nchini ni takwa na haja ya kweli ya wananchi wa Lebanon na kusisitiza kuwa matatizo ya kiuchumi na kisiasa hayawezi kupatiwa ufumbuzi bila ya kuwa na serikali. Wakati huo huo Sheikh Nabil Qaouq ambaye ni mjumbe wa Baraza Kuu la Hizbullah ameashiria kuwepo mgogoro wa kisiasa, kiuchumi na kijamii huko Lebanon na kusisitiza kuwa Walebanoni wote hivi sasa wanadhurika kutokana na kutoundwa serikali nchini.
Baada ya kuundwa bunge jipya la Lebanon, Saad Hariri tarehe 24 mwezi Mei mwaka huu aliarifishwa na Rais Michel Aoun wa Lebanon kuwa shakhsia anayepasa kuunda serikali mpya baada ya kuungwa mkono na mrengo wenye viti vingi bungeni.
Kizuizi kikuu kinachokwamisha kuundwa serikali mpya huko Lebanon ni hitilafu zilizopo kati ya makundi na vyama juu ya namna ya kugawana nyadhifa za wizara. Aidha mashinikizo ya nje khususan kutoka Saudi Arabia ni suala jingine linalokwamisha kupatiwa ufumbuzi hitilafu tajwa.