Wamisri kufanyika maandamano ya kupinga makubaliano ya Cairo na Riyadh
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i4918-wamisri_kufanyika_maandamano_ya_kupinga_makubaliano_ya_cairo_na_riyadh
Muungano wa kitaifa unaounga mkono serikali ya kidemokrasia na kupinga mapinduzi ya jeshi nchini Misri umetaka kufanyika maandamano kote nchini humo kulalamikia hatua ya Rais wa nchi hiyo ya kuipatia Saudi Arabia visiwa viwili vya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 12, 2016 11:51 UTC
  • Wamisri kufanyika maandamano ya kupinga makubaliano ya Cairo na Riyadh

Muungano wa kitaifa unaounga mkono serikali ya kidemokrasia na kupinga mapinduzi ya jeshi nchini Misri umetaka kufanyika maandamano kote nchini humo kulalamikia hatua ya Rais wa nchi hiyo ya kuipatia Saudi Arabia visiwa viwili vya nchi hiyo.

Muungano huo leo umetoa taarifa ukiyatolea mwito makundi yote nchini humo kushiriki katika maandamano siku ya Ijumaa tarehe 15 mwezi huu ili kuonyesha upinzani wao kwa hatua ya serikali ya Cairo ya kugawa ardhi ya Wamisri. Taarifa ya Muungano wa Kitaifa unaounga mkono serikali ya kidemokrasia na kupinga mapinduzi ya jeshi imeongeza kuwa, wananchi wa Misri kamwe hawatafumbia macho mamlala ya kujitawala ya visiwa viwili vya Sanafir na Tiran.

Wakati huo huo Chama cha Demokrasia ya Jamii pia kimetangaza kuwa, ofisi zake zote kote nchini Misri zimejiandaa kupokea malalamiko ya wananchi ili kuwasilisha mashtaka kisheria ya kupinga makubaliano ya kuainisha upya mipaka ya baharini kati ya Misri na Saudia.

Serikali ya Misri imetangaza rasmi kutia saini makubaliano ya mipaka ya baharini kati ya nchi hiyo na Saudi Arabia na kwa mujibu wa makubaliano hayo, Misri imeipatia Saudia visiwa viwili vya Sanafir na Tiran. Wananchi wa Misri wameikosoa na kuipinga vikali serikali kwa hatua yake ya kusaini makubaliano hayo na serikali ya Riyadh.