Kutolewa hukumu ya kunyongwa raia 103 wa Indonesia nchini Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i49279-kutolewa_hukumu_ya_kunyongwa_raia_103_wa_indonesia_nchini_saudia
Wizara ya Mambo ya Nje ya Indonesia imetoa taarifa ikisema kuwa, tokea mwaka 2011 hadi sasa utawala wa Saudia, umewahukumu kifo raia 103 wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 05, 2018 02:28 UTC
  • Kutolewa hukumu ya kunyongwa raia 103 wa Indonesia nchini Saudia

Wizara ya Mambo ya Nje ya Indonesia imetoa taarifa ikisema kuwa, tokea mwaka 2011 hadi sasa utawala wa Saudia, umewahukumu kifo raia 103 wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, raia hao wa Indonesia ambao kimsingi ni wafanyakazi wa kazi za ndani ya nyumba, tayari wamekwishanyongwa au wanasubiri kunyongwa. Kufichuliwa kwa ripoti hiyo ya kutisha kunaonyesha kwamba hatua za hivi karibuni za utawala wa Saudia ambao hivi karibuni pia ulimkata kichwa mwanamke mwingine wa Indonesia, sasa zimegeuka na kuwa mgogoro katika uhusiano wa Riyadh na Jakarta. Kufuatia jinai hizo za utawala wa Aal-Saud miji tofauti ya Indonesia imeshuhudia maandamano makubwa ya kulaani hukumu hizo za kunyongwa raia wa nchi yao na wameitaka serikali ya Jakarta kulalamikia vikali kadhia hiyo. Wiki iliyopita, Tuti Tursilawati msichana wa kazi za nyumbani nchini Saudia, bila ya kutaarifiwa familia yake wala ubalozi wa nchi yake, alikatwa kichwa nchini humo, kwa tuhuma za kile kilichotajwa na Saudia kuwa ni mauaji.

Waindonesia wakiandamana huku wakiwa wamebeba picha ya Tuti Tursilawati aliyekatwa kichwa hivi karibuni

Shirika la Kutetea Wahajiri nchini Indonesia ambalo limekuwa likitetea haki za wafanyakazi wa nchi hiyo, sambamba na kulaani jinai hiyo ya utawala wa Aal-Saud limetangaza kwamba, msichana huyo Tuti Tursilawati hakuhusika na mauaji, bali alikuwa akijitetea kutokana na mwajiri wake wa Kisaudi kutaka kumbaka. Makumi ya maelfu ya wanawake na wasichana kutoka nchi tofauti kama vile Bangladesh, Indonesia, Sri Lanka na Ufilipino wako nchini Saudia wakijishughulisha na kazi za nyumbani. Wanawake hao hukumbwa na vitendo vya ubakaji, kutopewa mishahara yao na kudhalilishwa na wanawafalme wa Saudia  waajiri wao wengine. Kuhusu hilo, kanali ya televisheni ya al-Alam hivi karibuni ilitangaza habari iliyoonyesha hali mbaya ya wafanyakazi wa kigeni nchini Saudia kwa kusema: "Nchini Saudia mbali na wafanyakazi wanaotoka mataifa ya Asia, wafanyakazi wanaotoka nchi za Afrika pia hufanyiwa vitendo vya ukatili na unyama katika mitaa au maeneo mengine kwa kupigwa na wakati mwingine kuuawa.

Ukatili uliokithiri wa watawala wa Saudia dhidi ya wafanyakazi wa kigeni

Hatua ya watawala wa Aal-Saud ya kuwashikilia maelfu ya wafanyakazi wa kigeni katika baadhi ya vituo visivyo na maji wala chakula na katika mazingira mabaya ya kiafya, imepelekea kuibuka maafa ya kibinaadamu. Mazingira mabaya ya maelfu ya wafanyakazi wa kigeni nchini Saudia ikiwemo mishahara midogo, miamala mibaya ya waajiri na kuwatumia kingono na kuwabaka, kwa hakika inaashiria mwendelezo wa utumwa dhidi yao." Watawala wa Saudia ambao hujiita kuwa wahudumu wa Haram mbili takatifu za Makkah na Madina katika miaka ya hivi karibuni wamehusika na jinai za kutisha nchini Yemen, Syria na mauaji ya kigaidi yanayotekelezwa kisiasa ambayo yamepelekea Waislamu duniani kutaka usimamizi wa maeneo hayo matukufu kusimamiwa na asasi za kimataifa za Kiislamu. Katika mazingira hayo, jinai za watawala na waajiri wa Saudi dhidi ya wafanyakazi wa kigeni wasio na utetezi na ambao walisafiri kuelekea Saudia kwa matarajio kwamba watapata ajira na usalama, zimegeuka na kuwa jambo la kawaida. Aidha vyombo vya mahakama nchini humo ambavyo vilitarajiwa kufanya uadilifu, kwa bahati mbaya haviwatetei hata kidogo wafanyakazi hao, na badala yake vinawaondolea hatia watawala na waajiri wanaotesa na kuwafanyia unyama wafanyakazi hao wa kigeni.

Viongozi wa Indonesia wakifuatilia haki za raia wao kwa watawala wa Saudia

Inaonekana kwamba serikali ya Indonesia kupitia mashinikizo ya waliowengi nchini humo, imelazimika kuanzisha uchunguzi wa kina kufuatia kitendo cha hivi karibuni cha kuuawa kwa kukatwa kichwa mfanyakazi wa kike wa nchi hiyo. Aidha kutolewa ripoti na Wizara ya Mambo ya Nje ya Indonesia juu ya hukumu za kunyongwa raia 103 wa nchi hiyo huko Saudia, bila shaka kutasaidia kuzuia kukaririwa mwenendo huo wa watawala wa Aal-Saud. Wajuzi wa masuala ya kisiasa nchini Indonesia wanaamini kuwa, kwa kuzingatia kulaaniwa na dunia nzima vitendo viovu vya watawala wa Saudia hususan kutokana na jinai zao za kutisha nchini Yemen, Syria na hata Iraq, serikali ya Jakarta  inatakiwa kutumia fursa hiyo kuweza kuwasilisha katika duru za kimataifa suala la mauaji ya wafanyakazi wake wa ndani huko Saudia ili sambamba na kulaaniwa kwake, jinai hizo zisikaririwe tena dhidi ya wafanyakazi wa kigeni walioko Saudia. Ni kwa msingi huo, ndio maana jumuiya za wafanyakazi na makundi mbalimbali ya kiraia nchini Indonesia katika hatua yao ya kulaani kitendo cha kukatwa kichwa mfanyakazi wa kike huko Saudia, sambamba na kutoa taarifa ya kulaani kitendo hicho, zimeitaka serikali ya Jakarta kutoa jibu kali kwa jinai za utawala wa Aal-Saud, kwa kuvunja makubaliano yote ya ushirikiano iliyotiliana saini na Riyadh.