"Saudia ilitumia programu ya udukuzi ya Israel kumfuatilia Kashoggi"
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i49374-saudia_ilitumia_programu_ya_udukuzi_ya_israel_kumfuatilia_kashoggi
Edward Snowden, afisa wa zamani wa Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani (NSA) amefichua nafasi ya utawala haramu wa Israel katika mauaji ya kikatili ya mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi yaliyofanywa na Riyadh nchini Uturuki mwezi uliopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 08, 2018 11:49 UTC

Edward Snowden, afisa wa zamani wa Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani (NSA) amefichua nafasi ya utawala haramu wa Israel katika mauaji ya kikatili ya mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi yaliyofanywa na Riyadh nchini Uturuki mwezi uliopita.

Snowden amesema Saudia yumkini ilitumia programu ya udukuzi ya Pegasus ya kampuni ya Israel ya NSO kumfuatilia Khashoggi, kabla ya kumuua. Amebainisha kuwa, simu erevu ya mmoja wa marafiki za Khashoggi ambaye yuko uhamishoni nchini Canada imeathiriwa na programu hiyo ya udukuzi ambayo Riyadh imekuwa ikitumia kuwafuatilia wakosoaji na wapinzani na utawala wa Aal Saud.

Amesema mbali na Khashoggi, Saudia inatumia programu hiyo kudukua mawasiliano ya marafiki wa mkosoaji huyo wa Saudia, ambaye mauaji yake yamezusha makelele mengi kutoka kila pembe ya dunia.

Edward Snowden aliwasilisha maelfu ya nyaraka za ujasusi na usalama za Marekani kwa waandishi wa habari mwaka 2013 na kukimbilia Russia

Taasisi ya utafiti ya Citizen Lab ya Canada pia imethibitisha kuwa, simu ya rununu ya Omar Abdulaziz, mwanaharakati wa Saudia anayeishi nchini Canada ililengwa na kuathiriwa na programu hiyo ya udukuzi ya Pegasus, ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mwandishi na mkosoaji wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi aliuawa na maafisa wa utawala wa Riyadh tarehe Pili Oktoba baada tu ya kuingia katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul.

Saudi Arabia inaendelea kukaidi wito wa jamii ya kimataifa unaoitaka Riyadh ikabidhi maiti ya mwandishi huyo wa habari aliyeuawa na kukatwa vipande vipande na kisha maiti yake ikapelekwa kusikojulikana.