Waandishi 100 wa habari waahidi kususia mkutano wa Mohammad Bin Salman
Waandishi wa habari 100 nchini Misri wametia saini hati ya kususia mkutano wa Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia atakapotembelea nchi hiyo.
Waandishi hao wa habari wamesema kuwa, kutokana na sababu za kibinaada na kitaalamu wameamua kususia mkutano wa mwanamfalme huyo wa Saudia. Wameongeza kwamba utawala wa kifalme wa Saudia hauyapi umuhimu kwa namna yoyote matukufu ya kibinaadamu ikiwemo haki ya kuishi raia wa Saudia na Misri. Kwa mujibu wa waandishi hao wa habari, sheria haina nafasi nchini Saudia na kwamba vyombo vya mahkama havina uhuru na wala haviaminiki kuweza kusimamia uadilifu.
Kadhalika waandishi wa habari wa Misri wameeleza sababu nyingine inayowafanya kususia mkutano na Mohammad Bin Salman mjini Cairo kuwa ni faili la mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari na mkosoaji wa utawala wa kifalme wa Saudia ndani ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki na wamesisitiza kwamba jinai hiyo ya wazi na ya kutisha ilisimamiwa na watawala wa Riyadh. Mohammad Bin Salman anaendelea na safari ya kuzitembeleza nchi kadhaa za Kiarabu kuanzia Imarati, Bahrain, Misri, Tunisia, Algeria na Mauritania, huku akikabiliwa na upinzani mkubwa wa raia wa nchi hizo.