Misri na Saudia zasema mzingiro dhidi ya Qatar utaendelea
(last modified Wed, 28 Nov 2018 07:41:07 GMT )
Nov 28, 2018 07:41 UTC
  • Misri na Saudia zasema mzingiro dhidi ya Qatar utaendelea

Saudi Arabia na Misri zimesema mzingiro na vikwazo zilivyoiwekea Qatar kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa vitaendelea kwa muda usiojulikana, licha ya Doha kuwasilisha lalama zake mbele ya mahakama za kimataifa na taasisi za Umoja wa Mataifa ili kushinikiza kuhitimishwa mzingiro huo.

Katika mkutano uliofanyika jana katika Ikulu ya Rais ya Ittihadiya mjini Cairo, Rais Abdulfattah al-Sisi wa Misri na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia, Mohammad bin Salman, walisisitizia haja ya kuendelezwa mzingiro huo wa kidhalimu dhidi ya jirani yao Qatar, huku wakibainisha kuwa, hali hiyo itaendelea kwa muda usiojulikana.

Kadhalika wawili hao wamedai kuwa nchi zao zitaendeleza jitihada za kukabiliana na kile walichokitaja kama 'uingiliaji wa Iran' katika masuala ya kieneo. 

Bin Salman anazitembelea nchi kadhaa za Afrika licha ya maandamano ya wananchi dhidi yake

Nchi za Kiarabu zinazoizingira Qatar yaani Saudia, Bahrain, Imarati na Misri zilitangaza kukata uhusiano wao na serikali ya Doha tarehe tano Juni mwaka jana baada ya nchi hiyo kukataa kuwa chini ya uongozi wa Saudia.

Serikali ya Doha imekuwa ikisisitiza kuwa, hatua hizo za vikwazo na mzingiro zinahesabika kuwa za jinai za kivita na kiuchumi na zinazolenga kuwaadhibu wananchi wa Qatar. Mbali na kukata uhusiano wao wa kidiplomasia na Doha, nchi hizo vibaraka pia zimefunga mipaka yao ya majini, ardhini na angani na Qatar. 

Tags