UN yaitaka Israel iondoke kwenye Miinuko ya Golan ya Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i49880-un_yaitaka_israel_iondoke_kwenye_miinuko_ya_golan_ya_syria
Kwa mara nyingine tena Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepasisha kwa wingi wa kura azimio la kuutaka utawala ghasibu wa Israel kuondoka katika eneo la Miinuko ya Golan la Syria ambalo umelikalia kwa mabavu kwa karibu nusu karne sasa.
(last modified 2026-04-28T05:09:17+00:00 )
Dec 01, 2018 04:35 UTC
  • UN yaitaka Israel iondoke kwenye Miinuko ya Golan ya Syria

Kwa mara nyingine tena Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepasisha kwa wingi wa kura azimio la kuutaka utawala ghasibu wa Israel kuondoka katika eneo la Miinuko ya Golan la Syria ambalo umelikalia kwa mabavu kwa karibu nusu karne sasa.

Azimio hilo lilipasishwa Ijumaa ya jana kwa idadi kubwa ya kura, ambapo nchi 99 zililiunga mkono azimio hilo, 10 zikipinga na 66 zikajizuia kupiga kura.

Azimio hilo la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopasishwa kwa wingi wa kura katika kikao cha jana mjini New York limeutaka utawala haramu wa Israel kuondoka mara moja katika eneo hilo la kistratajia, likisisitiza kuwa, hatua ya Tel Aviv ya kutekeleza sheria, mamlaka na utawala wake katika eneo hilo ni batili.

Azimio hilo kwa mara nyingine tena linathibitisha kuwa eneo la Golan linalokaliwa kwa mabavu na Israel ni milki ya Syria na imezitaja hatua zote za utawala wa Kizayuni katika eneo hilo kuwa ni batili na kinyume cha sheria.

Wanajeshi vamizi wa Israel katika Miinuko ya Golan ya Syria

Utawala wa Kizayuni wa Israel mwaka 1967 ulivamia na kulikalia kwa mabavu eneo la ardhi ya Syria la karibu kilomita mraba 1200 pamoja na Miinuko ya Golan na baada ya kupita muda utawala huo ukaliunganisha eneo hilo na ardhi unazozikalia kwa mabavu.  

Miinuko ya Golan ipo kusini magharibi mwa Syria katika mkoa wa Qunaitra na tangu mwanzoni mwa kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina eneo hilo lilimezewa mate na utawala wa Kizayuni kwa kuzingatia umuhimu wake wa kijiografia, kisiasa na kistratejia.