Qatar kujiondoa OPEC Januari 2019
Qatar imetangaza kuwa itajiondoa katika Shirika la Nchi Zinazouza Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC) mwezi ujao wa Januari 2019.
Uamuzi huo umetangazwa na Saad Sherida al-Kaabi Waziri wa Mafuta wa Qatar mapema leo Jumatatu. Shirika la Kitaifa la Mafuta la Qatar limethibitisha habari ya nchi hiyo kujiondoa OPEC, jumuiya ambayo inazileta pamoja nchi ambazo zinazalisha karibu nusu ya mafuta yote ya petroli duniani.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Doha, al-Kaabi amesema uamuzi wa kujiondoa OPEC unatokana na azma ya Qatar ya kuimarisha na kuongeza uzalishaji wa gesi asilia kutoka tani milioni 77 hadi milioni 110 kwa mwaka katika miaka ijayo.
Qatar ni nchi ya kwanza ya Ghuba ya Uajemi kutangaza kujiondoa katika OPEC.
Kwa zaidi ya mwaka moja sasa Qatar imekuwa chini ya mzingiro wa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri na Bahrain kufuatia hitilafu za kidiplomasia baina yake na nchi hizo za Kiarabu. Mapema wiki hii OPEC na Russia ambazo huzalisha asilimia 40 ya mafuta yote ya petroli duniani ziliafiki kupunguza uzalishaji ili kudhibiti bei.
Qatar hivi sasa ni mzalishaji mkubwa zaidi wa gesi asilia duniani LNG na huzalisha asilimia 30 ya gesi yote asilia duniani.