Njama mpya za Marekani za kuunda jeshi la kieneo nchini Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i50063-njama_mpya_za_marekani_za_kuunda_jeshi_la_kieneo_nchini_syria
Mkuu wa Jeshi la Marekani amesema kuwa nchi hiyo ina nia ya kuanzisha na kulipa mafunzo jeshi la watu 40 elfu mashariki mwa Syria kwa madai ya kuleta utulivu katika eneo hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 09, 2018 23:24 UTC
  • Njama mpya za Marekani za kuunda jeshi la kieneo nchini Syria

Mkuu wa Jeshi la Marekani amesema kuwa nchi hiyo ina nia ya kuanzisha na kulipa mafunzo jeshi la watu 40 elfu mashariki mwa Syria kwa madai ya kuleta utulivu katika eneo hilo.

Gazeti la Washington Post limemnukuu Jenerali Joseph Dunford akidai kuwa sababu ya uamuzi huo wa Marekani ni kuweko wanamgambo wa Daesh (ISIS) mashariki mwa Syria. Hata hivyo mkuu huyo wa jeshi la Marekani amekataa kusema hivi sasa kuna wanajeshi wangapi wa Marekani huko mashariki mwa Syria; alichosema tu ni kwamba kwa sasa hivi hakuna mpango wowote wa kuwaondoa wanajeshi hao huko nchini humo. 

Matamshi hayo ya viongozi wa Marekani yametolewa katika hali ambayo, Mkuu wa Jeshi la Russia, Jenerali Valery Gerasimov alisema siku ya Alkhamisi kwamba wanamgambo wa genge la kigaidi la Daesh sasa hivi wamebakia tu mashariki mwa Mto Furat na kusini mashariki mwa Syria ambako ndiko waliko wanajeshi wa Marekani. 

Magaidi wanaoungwa mkono na Marekani nchini Syria

 

Mgogoro wa Syria ulianzishwa kwa makusudi mwaka 2011 kwa wimbi kubwa la magaidi kuivamia nchi hiyo kutoka kila kona kwa uungaji mkono wa kila kitu wa Marekani, Saudi Arabia, Israel na waitifaki wao na shabaha yake kuu ni kubadilisha hali ya eneo la Mashariki ya Kati kwa manufaa ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Duru za kisiasa za Syria zinasema kuwa lengo hasa la njama hizo mpya za Marekani ni kujaribu kuigawa vipande vipande Syria kwa manufaa ya utawala wa Kizayuni na vile vile kuufanya mgogoro wa nchi hiyo uwe wa muda mrefu sana. 

Gazeti la al Binaa la Lebanon limeandika: Marekani inayaunga mkono magenge ya kigaidi kwa shabaha ya kuigawa vipande vipande Syria. Magenge ya kigaidi ambayo kwa miaka mingi sasa yameivamia Syria kwa uungaji mkono wa Marekani yanaendelea kupoteza nguvu zao, hivyo Washington imekusudia kuunda magenge mapya ya kigaidi ili kukwamisha juhudi za ukombozi wa ardhi yote ya Syria. Kuendelea Marekani kuwekeza kwa ajili ya magaidi wa Idlib na kung'ang'ania Marekani msimamo wake wa kulitaka jeshi la Syria na waitifaki wake kusimamisha mashambulizi dhidi ya magenge la kigaidi hasa la Jabhat al Nusra ambalo sasa hivi linajiita Hay'at Tahrirush Sham ni ushahidi wa wazi wa njama hizo za Marekani. Kwa mfano hapa panazuka maswali kadhaa ambayo Wamarekani kamwe hawako tayari kuyajibu nalo ni kwamba, je, inawezekano polisi ya Chicago huko Marekani kufikia makubaliano ya kusimamisha vita na wahalifu? Je, jeshi la Marekani linaweza kusimamisha vita na kutowashambulia magaidi wanaoshambulia ikulu ya nchi hiyo White House na baraza la Congress? Kwa nini Marekani haiko tayari kutekeleza nchini Syria hata sheria zake mwenyewe inazozitekeleza huko Marekani kuhusu magaidi? Kiujumla ni kwamba, kushindwa njama za Wamarekani nchini Syria na kupata nguvu serikali ya Damascus kiasi cha kukomboa takriban ardhi zote za nchi hiyo, kumevuruga njama zote za maadui waliokuwa wanaota kuigawa vipande vipande nchi hiyo ya Kiarabu. Ukweli wa mambo ni kuwa shabaha kuu ya maadui ni kuidhoofisha Syria, kuisambaratisha nchi hiyo na hatimaye kupora utajiri wake.

Maadui wa ubinadamu wanafanya kila njia kumwaga damu za watu wasio na hatia 

 

Kwa kuzingatia yote hayo tutaona kuwa, muungano wa eti kupambana na ugaidi unaoongozwa na Marekani, hivi sasa unafanya njama za kubadilisha majina ya magaidi waliowamimina huko Syria na kuhalalisha njama zao hizo kwa madai ya eti kupambana na magaidi wa Daesh. Udadisi mwingine walio nao watu wengi ni kwamba, vipi Marekani inajipa uthubutu wa kuvamia nchi ya watu bila ya idhini na kufikia hata kutangaza hadharani kuwa inaunda jeshi la kieneo la eti kupambana na magaidi ambao Wamarekani wenyewe wanakiri mara kwa mara kuwa ni wao ndio walioyaanzisha magenge hayo ya kikatili kwa ajili ya kuzidhoofisha nchi zisizokubali kuburuzwa kama Syria? Ni jambo lisilo na shaka kwamba siasa za Marekani ni kuchochea machafuko na kutoa mwanya kwa magaidi kuzidi kufanya jinai kieneo na kimataifa kwa lengo la kujinufaisha binafsi.