Qatar: Baraza la (P)GCC halina uwezo na limebaki limeemewa
(last modified Sat, 15 Dec 2018 14:26:40 GMT )
Dec 15, 2018 14:26 UTC
  • Qatar: Baraza la (P)GCC halina uwezo na limebaki limeemewa

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar amesema kuwa, Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi limebaki kimuundo tu lakini taratibu zake kiutendaji hazitekelezeki.

Muhammad bin Abdurrahman Aal-Thani amesema hayo leo mjini Doha, Qatar katika hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa 18 wa Kimataifa wa Doha (Jukwaa la Doha-2018) na kusema bayana kwamba, Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi pamoja na Katibu Mkuuu wakke hawana mamlaka yoyote.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar amesema kuwa, kuna haja ya kufanyika marekebisho na kuweko nidhamu mpya pamoja na mikakati ya lazima kwa nchi zote wanachama.

Kwa upande wake Amir wa Qatar Tamim bin Hamad Aal-Thani akihutubia hafla ya ufunguzi wa mkutano huo wa kimataifa, aliashiria kuzingirwa nchi yake na Saudi Arabia, Imarati na Bahrain na kusisitiza kwamba, misimamo ya Doha kuhusiana na mgogoro wa Ghuba ya Uajemi haijabadilika na nchi hiyo ingali inasisitizia kufanyika mazungumzo na kutokuweko uingiliaji katika masuala ya ndani ya nchi nyingine.

Muhammad bin Abdurrahman Aal-Thani, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar

Tarehe 5 Juni mwaka uliopita wa 2017, Saudi Arabia, Imarati, Bahrain pamoja na Misri zilivunja uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar kwa sababu ya serikali ya Doha kutofuata muelekeo wa nchi za Kiarabu zinazoongozwa na Saudia.

Lakini mbali na kuiwekea vikwazo Qatar, nchi hizo zilifungia pia Doha mipaka yao ya ardhini, baharini na angani, mzingiro ambao ungali unaendelea hadi leo. Masharti yote yaliyotolewa na nchi hizo kwa ajili ya kurejesha tena uhusiano wao na nchi hiyo, yamekataliwa na serikali ya Doha.

Tags