CBS: Misri na Israel zina ushirikiano wa karibu wa kijeshi
(last modified Sat, 05 Jan 2019 07:57:24 GMT )
Jan 05, 2019 07:57 UTC
  • CBS: Misri na Israel zina ushirikiano wa karibu wa kijeshi

Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri ameiomba kanali ya televisheni ya CBS ya Marekani kutorusha hewani mahojiano iliyomfanyia, ambapo alifichua kuhusu uhusiano wa karibu wa kijeshi wa nchi hiyo na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mahojiano hayo ya kipindi cha 60 Minutes cha runinga ya CBS yanatarajiwa kupeperushwa hewani Jumapili ya kesho. Hata hivyo balozi wa Misri nchini Marekani ameipigia simu CBS, na kuiomba isirushe hewani mahojiano hayo, ombi ambalo limekataliwa.

Katika mahojiano hayo, Rais al-Sisi alimuambia mtangazaji wa CBS, Scott Pelley kwamba, jeshi la Misri linashirikiana kwa karibu na jeshi la utawala haramu wa Israel katika 'vita dhidi ya ugaidi' katika Peninsula ya Sinai.

Alipoulizwa iwapo uhusiano wa sasa kati ya Misri na Israel ndio wa karibu zaidi katika kipindi chote cha historia, Rais wa Misri alisema 'Ni kweli, tunashirikiana na Israel katika mambo mengi."

Rais Abdul Fattah al-Sisi wa Misri

Mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka uliomalizika 2018, gazeti la Al-Araby Al-Jadeed linalochapishwa nchini Uingereza liliripoti kuwa Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia Muhammad bin Salman na Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri wamekuwa wakiendesha kampeni ya pamoja ya kuwashawishi viongozi wa nchi zingine za Kiarabu waanzishe uhusiano wa karibu na Israel, huku wakiendelea kutatua tofauti za kisiasa na utawala huo haramu wa Kizayuni.

Itakumbukwa kuwa, Jordan na Misri ni nchi mbili za Kiarabu zilizotia saini mkataba wa amani ulioidhinisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi baina yao na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Tags