Israel yakiri kuwapa msaada wa silaha wapinzani wa serikali ya Syria
(last modified Wed, 16 Jan 2019 04:28:38 GMT )
Jan 16, 2019 04:28 UTC
  • Israel yakiri kuwapa msaada wa silaha wapinzani wa serikali ya Syria

Mkuu wa Majeshi ya Utawala wa Kizayuni wa Israel amekiri kuwa utawala huo umekuwa ikiwapa silaha wapinzani wa serikali ya Syria.

Gadi Eizenkot Mkuu wa Majeshi ya Israel anayeondoka, katika mahojiano na gazeti la  Sunday Times la Uingereza amesema Israel imehusika katika vita nchini Syria kwa kuunga mkono makundi ya waasi ambapo imewapa silaha.

Wanajeshi wa serikali ya Syria wamenasa silaha zilizotengenezwa Marekani na katika utawala haramu wa Israel ambazo zilikuwa zinatumiwa na magaidi wakufurishaji katika mkoa wa Dara'a kusini maghairbi mwa nchi hiyo.

Mwezi Juni mwaka jana Afisa mmoja wa utawala wa Kizayuni wa Israel alikiri kuwa, jeshi la utawala huo linawapa matibabu magaidi na wapinzani wa serikali ya Syria ambao wanajeruhiwa vitani nchini Syria na kuutaja msaada huo kuwa eti ni 'kazi takatifu zaidi'.

Gadi Eizenkot

Kwa mujibu wa gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post, Kapteni Aviad Camisa, Naibu Mkuu wa Kitengo cha Matibabu katika Divisheni ya 210 ya Bashan, alikiri wazi wazi kuwa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limekuwa likiwapa matibabu magaidi kutoka Syria. Alisema magaidi hao wanatibiwa katika Miinuko ya Golan ya Syria ambayo sasa inakaliwa kwa mabavu na Israel. Camisa alisema, Israel hutoa huduma bora, za haraka na za kisasa kabisa kwa magaidi waliojeruhiwa vitani nchini Syria.

Tokea mwaka 2011, Syria imekuwa ikikabiliana na hujuma kubwa ya magaidi wanaopata himaya ya madola ya kigeni hasa Saudi Arabia na Marekani kwa lengo la kuiangusha serikali ya nchi hiyo kwa maslahi ya utawala haramu wa Israel.

Tags