Palestina yalaani chokochoko mpya za Israel dhidi ya Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i51040-palestina_yalaani_chokochoko_mpya_za_israel_dhidi_ya_syria
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) na harakati ya Jihad al-Islami ya Palestina zimelaani mashambulizi mapya ya kichokozi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 22, 2019 04:03 UTC
  • Palestina yalaani chokochoko mpya za Israel dhidi ya Syria

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) na harakati ya Jihad al-Islami ya Palestina zimelaani mashambulizi mapya ya kichokozi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Syria.

Msemaji wa Hamas, Abdul-Latif al-Qanou amesema hujuma ya usiku wa kuamkia leo ya jeshi la Israel dhidi ya Syria imedhihirisha kwa mara nyingine tena kwamba utawala huo haramu ndio adui na tishio kuu kwa umoja wa umma wa Kiislamu.

Wakati huohuo, msemaji wa Jihad al-Islami, Davoud Shahab ameandika kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, lengo la uchokozi huu mpya wa Wazayuni ni kujaribu kuvuruga usalama na uthabiti wa Syria ambao unaelekea kutengenea.

Huku hayo yakiarifiwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imeliandikia barua Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikilitaka lichukue hatua za makusudi kukomesha chokochoko hizo za Israel dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Nembo ya Jihad Islam

Usiku wa kuamkia leo utawala wa Kizayuni wa Israel umefanya mashambulizi ya makombora ukilenga mji mkuu wa Syria, Damascus. Hata hivyo mfumo wa ulinzi wa anga wa Syria umetungua makombora hayo ya Israel.

Hujuma ya jana usiku ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Syria ni ya tatu tangu mwaka huu mpya wa 2019 uanze.