Syria yaalikwa kushiriki kikao cha mabunge ya nchi za Kiarabu
Duru za Jordan zinaarifu kuwa Atef Tarawneh, spika wa bunge la Jordan amemwalika spika mwenzake wa Syria Hammouda Sabbagh, kushiriki katika kongamano la 29 la mabunge ya nchi za Kiarabu ambalo limepangwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi Machi huko Amman mji mkuu wa Jordan.
Wito kwa Syria kwa ajili ya kushiriki kikao hicho ambayo ni sehemu muhimu ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League), ni ishara ya wazi kwamba kuna juhudi za makusudi zinazofanyika kwa shabaha ya kuirejesha katika jumuiya hiyo baada ya uanachama wake kusimamishwa kwa muda mwaka 2011. Matukio ya eneo kufuatia ushindi mkubwa na wa mara kwa mara wa serikali ya Syria dhidi ya makundi ya kigaidi na kuendelea kuimarika nafasi ya Rais Bashar Asad katika upeo wa kieneo na kimataifa ni mambo ambayo yamepelekea kubadilika misimamo ya kieneo na kimataifa kwa manufaa ya Syria. Mabadiliko hayo ya misimamo yanadhihirika wazi hasa miongoni mwa nchi za Kiarabu ambazo zimekuwa zikishirikiana kwa karibu na madola ya Magharibi dhidi ya serikali ya Damascus. Mabadiliko hayo ambayo yamekuwa yakionekana wazi katika wiki za hivi karibuni katika serikali ya Jordan na serikali nyingine za Ghuna ya Uajemi kuihusu Syria, yanaweza kutathminiwa katika mtazamo huo.
Hatua ya kiuhasama ya kusimamisha uanachama wa Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilichukuliwa katika hali ambayo nchi hiyo ni moja ya waasisi wa jumuiya hiyo. Jumuiya ya Arab League ilibuniwa tarehe 22 Machi 1945 na nchi 6 waasisi ambazo ni Misri, Saudi Arabia, Iraq, Syria, Lebanon na Jordan, ambapo hivi sasa ina nchi wanachama 22 za Kiarabu (zikiwemo 10 za Kiafrika na 12 za Asia). Licha ya Jumuiya hiyo kubuniwa na nchi kadhaa za Kiarabu lakini imeathiriwa na kudhibitiwa na baadhi ya nchi vibaraka ambazo zinaegemea upande wa Magharibi na hivyo kuathiri pakubwa utendeji wa jumuiya hiyo kwa madhara ya nchi wanachama. Katika kuendeleza hatua zake zilizojaa makosa, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilichukua uamuzi wa kusimamisha uanachama wa Syria katika jumuiya hiyo na hatimaye kuyaunga mkono makundi ya kigaidi kwa madhumuni ya kuitoa madarakani serikali halali ya rais Bashar al- Asad. Hatua hiyo ya kiuhasama na uchokozi ilichukuliwa kinyume kabisa na hati ya umoja huo yenyewe inayopinga kuingiliwa mambo ya ndani ya nchi nyingine wanachama.
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ambayo kidhahiri ilibuniwa kwa madhumuni ya kuimarisha ushirikiano na uthabiti wa ulimwengu wa Kiarabu kwa muda mrefu sasa imekuwa ni kituo cha watawala waovu wa Kiarabu wakiwemo wa Saudi Arabia, kuendeleza siasa zao za uingiliaji wa mambo ya ndani ya nchi nyingine za Kiarabu na kueneza ugaidi katika eneo hili muhimu la Mashariki ya Kati. Udhaifu wa jumuiya hiyo katika kutekeleza majukumu yake ndio umeipelekea kushindwa kutatua matatizo na changamoto muhimu za kieneo likiwemo suala la Palestina na migogoro ya Syria, Yemen na Libya. Mwenendo huo hasi wa Jumuiya ya Kiarabu umeifanya ifuatilie tu mambo ya pembeni na kusahau jukumu lake la msingi la kutatua changamoto muhimu za nchi za Kiarabu zikiwemo za kiuchumi na kijamii. Mazingira hayo bila shaka yanatoa udharura wa Jumuiya hiyo kujirudi na kulazimika kutazama upya siasa zake mbovu za miaka ya hivi karibuni dhidi ya Syria, nchi ambayo daima imekuwa ikufanya juhudi za kuleta umoja na mshikamano katika ulimwengu wa Kiarabu. Mtazamo mpya wa nchi za Kiarabu na uamuzi wao wa kuanzisha tena uhusiano na Syria pamoja na kufanyika juhudi za kufidia makosa yaliyofanyika huko nyuma, bila shaka ni namna moja ya nchi za Kiarabu kukiri nafasi muhimu na maalumu ya Syria katika eneo na upeo wa kimataifa.