Mwanajeshi Mzayuni atwangwa risasi na mwanamapambano wa Palestina + Video
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i51315-mwanajeshi_mzayuni_atwangwa_risasi_na_mwanamapambano_wa_palestina_video
Tawi la kijeshi la harakati ya Jihadul Islami ya Palestina jana Jumapili lilisambaza video inayoonesha jinsi mtunga shabaha stadi (sniper) wa harakati hiyo alivyomdungua kwa risasi mwanajeshi Mzayuni ambaye alikuwa akiwashambulia kwa risasi waandamanaji wa Palestina.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Feb 03, 2019 21:34 UTC

Tawi la kijeshi la harakati ya Jihadul Islami ya Palestina jana Jumapili lilisambaza video inayoonesha jinsi mtunga shabaha stadi (sniper) wa harakati hiyo alivyomdungua kwa risasi mwanajeshi Mzayuni ambaye alikuwa akiwashambulia kwa risasi waandamanaji wa Palestina.

Brigedi za al Quds, tawi la kijeshi la harakati ya Jihadul Islami ya Palestina limesema katika taarifa yake kwamba, tukio hilo limetokea katika mpaka wa Ghaza na ardhi nyingine za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa "Falastin al Yaum" afisa huyo wa kijeshi Mzayuni alidunguliwa kwa risasi na mtunga shabaha stadi wa Jihadul Islami, lakini risasi hiyo ilipiga kwenye kofia yake na kuzuia kuangamizwa.

Kofi ya mwanajeshi Mzayuni iliyochakazwa kwa risasi ya mwanamapambano wa Palestina

 

Kwa upande wake, televisheni ya al Mayadeen ya nchini Lebanon imetangaza kuwa, harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Jihadul Islami imetangaza kuhusika na opereshenei hiyo. Msemaji wa harakati hiyo, Musab al-Barim ameiambia televisheni hiyo kwa njia ya simu kwamba, adui Mzayuni anafanya vitendo vya kikatili mno vya kigaidi dhidi ya Wapalestina hivyo ni haki ya Wapalestina kujibu mashambulio ya Wazayuni hao.

Daud Shahab, mwanachama mwingine wa ngazi za juu wa Jihadul Islami naye amesema, makundi yote ya Palestina yana kauli moja kuhusu ulazima wa kujibu jinai zote za Wazayuni. Amesema, tunapoiangalia video inayohusiana na tukio hilo ambayo inamuonesha mwanajeshi Mzayuni akiwashambulia kwa risasi wananchi wa Palestina, tutatambua kuwa ni haki ya Wapalestina kujibu jinai hizo za Wazayuni. 

Itakumbukwa kuwa tarehe 22 mwezi ulioisha wa Januari 2019, msemaji wa jeshi la Israel, Avichay Adraee alisambaza picha ya kofia ya mwanajeshi huyo Mzayuni uliyochakazwa kwa risasi ya mwanamapambano huyo wa Palestina.