Wapinzani wanaozuiliwa Saudia waanza mgomo wa kula
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i51660-wapinzani_wanaozuiliwa_saudia_waanza_mgomo_wa_kula
Shirika la kutetea haki za wafungwa la Prisoners of Conscience limetangaza kuwa, idadi kubwa ya wapinzani wanaozuiliwa katika jela za kuogofya za Saudi Arabia wameanza mgomo wa kula, kulalamikia hali ngumu na mateso wanayopitia wakiwa kizuizini.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Feb 19, 2019 15:45 UTC
  • Wapinzani wanaozuiliwa Saudia waanza mgomo wa kula

Shirika la kutetea haki za wafungwa la Prisoners of Conscience limetangaza kuwa, idadi kubwa ya wapinzani wanaozuiliwa katika jela za kuogofya za Saudi Arabia wameanza mgomo wa kula, kulalamikia hali ngumu na mateso wanayopitia wakiwa kizuizini.

Kwa mujibu wa shirika hilo, miongoni mwa wanaharakati mashuhuri waliojiunga na kampeni hiyo ya kususia kula ni pamoja na Abdulkareem al-Khodor ambaye ni mwanachama wa shirika la kutetea haki za binadamu la Saudi Civil and Political Rights Association (ACPRA), Abdullah al-Hamid, Abdulrahman al-Hamid, Fawzan al-Harbi na Mohammad Fahad al-Qahtani.

Kampeni hiyo ya wafungwa wa kisiasa nchini Saudia kususia kula haina muda maalumu.

Wanaharakati 2,613 wakiwemo wanazuoni wa Kiislamu, majaji, waandishi wa habari na wakili wanaoonekana kuwa wapinzani wa utawala huo wa kiukoo wanaendelea kuzuiliwa katika mazingira magumu katika jela za Aal-Saud.

Baadhi ya wanaharakati wanawake wanaozuiliwa nchini Saudia

Vilevile katika miaka ya hivi karibuni serikali ya Riyadh imewakamata na kuwazuilia makumi ya wanaharakati wa kike wa kutetea haki za wanawake na kuwatuhumu kuwa wameisaliti nchi, kudhuru maslahi ya taifa na kuwaunga mkono kifedha na kiroho maadui wa nchi hiyo.

Shirika la kutetea haki za binadamu la al Qist lilichapisha ripoti mpya hivi karibuni na kufichua kwamba, wafungwa wa kike nchini Saudia wanafanyiwa mateso ya kinyama na kwamba baadhi ya mateso hayo yanasimamiwa na watu wa karibu kwa Mrithi wa Ufalme wa nchi hiyo, Muhammad bin Salman.