UN: Israel imefanya jinai dhidi ya binadamu Palestina
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameripoti kuwa, Israel imefanya jinai dhidi ya binadamu katika kukandamiza maandamano ya raia wa Ukanda wa Gaza.
Ripoti iliyotolewa jana na wataalamu wa Umoja wa Mataifa imesema, ushahidi unaonesha kuwa utawala wa Israel ulifanya jinai dhidi ya binadamu wakati wa kukabiliana na maandamano ya amani ya mwaka 2018 ya Wapalestina katika eneo la Ukanda wa Gaza.
Ripoti hiyo imesema kuwa, walenga shabaha wa Israel walikuwa wakiwapiga risasi kwa makusudi watoto wadogo, wafanyakazi wa uokoaji na waandishi wa habari.
Mkuu wa tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu matukio ya Ukanda wa Gaza, Santiago Canton pia ametoa taarifa akisema askari wa Israel wamekiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kibinadamu. Canton amesisitiza kuwa, uhalifu huo unatambuliwa kuwa ni jinai dhidi ya binadamu.
Timu hiyo ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa imekusanya ripoti ya jinai dhidi ya binadamu zilizofanywa na walenga shabaha na makamanda wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel ambayo imekabidhiwa kwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet.
Tangu tarehe 30 Machi mwaka jana Wapalestina wa Ukanda wa Gaza wamekuwa wakifanya maandano yaliyopewa jina la Haki ya Kurejea katika kila siku za Ijumaa. Tangu wakati huo jeshi la Israel limekuwa likishambulia maandamano hayo ya amani na hadi sasa limeua raia wasiopungua 260 wa Palestina na kujeruhi wengine wasiopungua elfu 27.