Misri yajiondoa katika muungano dhidi ya Iran, Marekani yachanganyikiwa
Serikali ya Misri imetangaza uamuzi wa kujiondoa katika muungano dhidi ya Iran unaojulikana kama "NATO ya Kiarabu" ambao unaongozwa na Marekani.
Duru za kidiplomasia zimeliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa, hatua ya Misri itakuwa ni pigo kubwa kwa utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani na sera yake dhidi ya Iran. Hii ni kwa sababu Misri inahesabiwa kuwa moja kati ya nchi muhimu zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu. Taarifa zinasema Misri iliifahamisha Marekani kuhusu uamuzi wake huo kabla ya mkutano uliofanyika mjini Riyadh, Saudi Arabia kuhusu muungano huo wa "NATO ya Kiarabu" ambayo jina lake limependekezwa kuwa "Muungano wa Usalama Mashariki ya Kati au MESA.
Marekani inalenga kutumia MESA ili kuzichochea nchi za Kiarabu kutumia njia za kiusalama, kisiasa na kiuchumi katika kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Imedokezwa kuwa Misri imejiondoa katika muungano huo baada ya kubaini kuwa Marekani haiwezi kuaminika katika muungano kama huyo na pia wakuu wa Cairo wanaonekana kutokuwa na hamu ya kuzidisha uhasama na Iran.
Afisa mmoja wa Saudi Arabia ambaye hakutaka jina lake litajwe amekiri kuwa jitihada za Marekani za kuanzisha muungano dhidi ya Iran haziendi vizuri.
Pendekezo la kuanzishwa "NATO ya Kiarabu" liliwasilishwa na Marekani pamoja na Saudia mwaka 2017 lakini hadi sasa halijazaa matunda.