Jenerali Mzayuni akiri nguvu za makombora za HAMAS huko Palestina
Jenerali mmoja Mzayuni amekiri kuwa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ina nguvu kubwa za makombora ambazo zinaweza kusambaratisha maisha ya wakazi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Gazeti la Kizayuni la Hayom liliripoti habari hiyo jana (Jumatatu) na kumnukuu Jenerali Israel Ziv ambaye pia alikuwa kamanda wa kikosi cha Ghaza cha jeshi la Israel akizungumzia nguvu za makombora za wanamuqawama wa Palestina ambazo kila uchao zinazidi kuongezeka na kusema kuwa, HAMAS hivi sasa ina jeshi lililojipanga vizuri na lina uwezo mkubwa wa kujihami na kushambulia.
Jenerali huyo Mzayuni ameongeza kuwa, kadiri siku zinavyopita ndivyo HAMAS inavyozidi kukaribia kufanikisha malengo yake na kwamba stratijia iliyotumiwa na harakati hiyo katika maandaano ya kila siku ya Ijumaa ya "Haki ya Kurejea" pamoja na makombora yaliyolengwa na HAMAS katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ni uthibitisho kuwa makamanda wa harakati hiyo wamejipanga vizuri kukabiliana na Israel.
Amesema harakati ya HAMAS imekuwa tishio lisilovumilika tena na kuna wajibu wa kuliondoa, hivyo kuna wajibu wa kubadilika siasa za Israel kuhusu suala hilo bila ya kujali usahihi na utovu wa usahihi wake.
Kabla ya hapo, Yahya Sinwar, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS alikuwa ameonya kwamba kama Israel itazusha vita vingine Ukanda wa Ghaza basi majibu ya HAMAS yatakuwa makali kiasi kwamba Wazayuni hawatalazimika kuhamisa watu karibu na Ukanda wa Ghaza tu, bali miji mingine yote ikiwemo Asqalan (Ashkelon) na Tel-Aviv itabidi watu wake wahamishwe.