Kuwait yataka Israel itimuliwe katika Jumuiya ya Mabunge
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i53269-kuwait_yataka_israel_itimuliwe_katika_jumuiya_ya_mabunge
Spika wa Bunge la Kuwait amesisitiza juu ya kuendelezwa juhudi za kutimuliwa utawala haramu wa Israel kutoka katika Jumuiya ya Mabunge kutokana na jinai zake unazozitenda.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
May 04, 2019 10:31 UTC
  • Kuwait yataka Israel itimuliwe katika Jumuiya ya Mabunge

Spika wa Bunge la Kuwait amesisitiza juu ya kuendelezwa juhudi za kutimuliwa utawala haramu wa Israel kutoka katika Jumuiya ya Mabunge kutokana na jinai zake unazozitenda.

Marzouq al-Ghanim amesisitiza kwa mara nyingine tena kwamba, kuna udharura kwa Bunge la Kiarabu kufungamana na suala la kupinga kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Spika wa Bunge la Kuwait amesema kuwa, udhaifu na migawanyiko ya nchi za Kiarabu imeifanya serikali ya Marekani itangaze na kuitambua rasmi Beitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala dhalimu wa Israel na kuhamishia ubalozi wake katika mji huo kutoka mjini Tel Aviv.

Aidha ameongeza kuwa, udhaifu na mifarakano iliyoko katika nchi za Kiarabu imeifanya serikali ya Marekani pia itambue rasmi umiliki wa Israel kwa miinuko ya Golan ya Syria.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel

Amesema kuwa, Bunge la Kuwait linaendeleza juhudi zake kuhakikisha kuwa, utawala wa kibaguzi wa Israel unatimuliwa katika Jumuiya ya Mabunge.

Spika wa Bunge la Kuwait amesisitiza pia kwamba, vita dhidi ya ugaidi vinapaswa kuanza kwa kuipatia ufumbuzi kadhia ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, harakati za kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na nchi za Kiarabu zimeongezeka zaidi baada ya Benjamin Netanyahu kufanya safari nchini Oman Oktoba mwaka jana, hatua ambayo ilipelekea Oman iandamwe na ukosoaji mkubwa.