Amir wa Qatar: Tutaendelea kuliunga mkono taifa madhulumu la Palstina
Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani amesema kuwa, msimamo wa Doha wa kuunga mkono na kutetea haki za taifa madhulumu la Palestina ni thabiti na usiotetereka.
Amir wa Qatar amesema hayo leo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Ismail Hania, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na kueleza kwamba, serikali ya Doha haitaacha kuunga mkono juhudi za kila upande zenye lengo la kupunguza machungu na masaibu ya taifa la Palestina.
Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani amesisitiza kuwa, nchi yake itaendelea kuliunga mkono kwa nguvu zake zote taifa la Palestina na wananchi wake wanaotaabika kutokana na siasa za utawala ghasibu wa Israel.
Kwa upande wake Ismail Hania, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amepongeza misimamo ya serikali ya Qatar na Amir wa nchi hiyo Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani.
Aidha ameishukuru serikali ya Qatar kwa msaada wake wa hivi karibuni wa dola milioni 480 kwa Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi wa Jordan na Ukanda wa Gaza.
Utawala wa Kizayuni wa Israel unalizingira eneo la Ukanda wa Gaza tangu mwaka 2006 wakati Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS iliposhinda uchaguzi wa Bunge la Palestina. Tangu wakati huo Israel ilizuia kuingizwa bidhaa zote muhimu katika eneo hilo kama vile chakula, madawa, vifaa vya ujenzi na kadhalika.