Hamas yataka Wapalestina wawe wabunifu katika kupambana na Wazayuni
(last modified Fri, 14 Jun 2019 06:39:11 GMT )
Jun 14, 2019 06:39 UTC
  • Hamas yataka Wapalestina wawe wabunifu katika kupambana na Wazayuni

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeitaka serikali na wananchi wa Palestina kuwa na ubunifu wa kitaifa katika kukabiliana na siasa za kibeberu za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Abdul-Hakim Hanini, mmoja wa viongozi waandamizi wa HAMAS alisema jana Alkhamisi kwamba kwa vile utawala wa Kizayuni unaendeleza siasa zake za kidhulma, kuteka ardhi za Wapalestina na kuzidi kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, ni wajibu kwa wananchi wa Palestina kuwa na msimamo mmoja wa kitaifa ili kuzuia Wazayuni wasiendelee kupora ardhi za Wapalestina.

Ameongeza kuwa, hivi sasa Wapalestina wako katika kipindi nyeti na muhimu mno na haitoshi kulaani kwa maneno tu jinai zinazofanywa na Wazayuni, bali inabidi wachukue hatua za kivitendo za kulinda haki zao.

Utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya jinai kubwa dhidi ya Wapalestina

 

Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS vile vile amesema ni wajibu kwa makundi yote ya Palestina kutumia nguvu na uwezo wao wote kuzuia mpango wa Wazayuni wa kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Siku chache zilizopita, David Friedman, balozi wa Marekani katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu alidai kuwa Israel ina haki ya kutwaa baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. 

Madai hayo mapya ya Marekani yametolewa katika kipindi cha chini ya miezi miwili tangu Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon aliposema baada ya Trump kutangaza rasmi kuwa milima ya Golan ya Syria ni mali ya Israel kwamba, kitendo cha ulimwengu wa Kiarabu na wa Kiislamu cha kunyamazia kimya hatua hiyo ya Trump, kitepelekea kushuhudiwa hatua nyingine mbaya ya Trump ambapo sasa atasema, Ukingo wa Magharibi nao ni ardhi ya Israel.

Tags