HAMAS: Vitisho vya Netanyahu vinatuzidishia azma na irada ya muqawama
(last modified Fri, 05 Jul 2019 12:50:51 GMT )
Jul 05, 2019 12:50 UTC
  • HAMAS: Vitisho vya Netanyahu vinatuzidishia azma na irada ya muqawama

Mjumbe mmoja wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu Palestina (HAMAS) amesema kuwa, vitisho vya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni vinauzidishia muqawama azma na irada ya kuendelea mbele na njia yake tukufu.

Khalil al-Hayya, amesisitiza kuwa, muqawama wa Palestina umepiga hatua kubwa katika uga wa uwezo na itikadi na kwamba hatua ijayo ni ya kuimarisha uwezo zaidi wa kukabiliana na wavamizi wa Kizayuni katika nyuga zote. Wiki iliyopita Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni alikiri kutokuwa na natija mashinikizo ya serikali yake dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Ghaza na wakati huo huo alitoa vitisho kwamba iwapo hatua zake hizo zitaendelea kutozaa matunda, basi Tel Aviv itatumia hatua ya kijeshi dhidi ya eneo hilo lililozingirwa kila upande.

Khalil al-Hayya, Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu Palestina (HAMAS)

Wakati huo huo Salah al-Bardawil, mjumbe mwingine wa Ofisi ya Kisiasa wa Harakati ya Hamas ameitaka harakati ya Fat'h kuendesha mazungumzo ya moja kwa moja kwa lengo la kutatua tofauti zilizopo ili kufikiwa hatua mpya ya kukabiliana na mpango wa Marekani wa Muamala wa Karne. Hii ni katika hali ambayo Nabil Shaath, Mshauri wa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina wiki iliyopita pia alitoa pendekezo kwa harakati ya HAMAS ya kufanyika uchaguzi na kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa ya Wapalestina wote. 

Tags